Ukitaka kujua tabia za jamii ya watu wowote wale, angalia tabia za watu ambao ni maarufu au viongozi kwenye jamii hizo.

Hao ndiyo wanawakilisha vizuri tabia za watu wote kwenye jamii hiyo kwa ujumla.

Na hilo linaweza kuwa limetengenezwa kwa njia mbili;

Moja, jamii nzima ndiyo ina sifa hizo na wachache ambao wanazo kwa kiwango cha juu ndiyo wanapata umaarufu na nafasi za juu za uongozi.

Mbili; watu wanakuwa na tabia fulani na wanapata nafasi za juu na hivyo kuwa na ushawishi kwa wengine kuwa na tabia za aina hiyo pia.

Wakati mwingine yote yanakwenda kwa pamoja, jamii inakuwa na tabia fulani, wachache wanaoziweza vizuri tabia hizo wanapata nafasi za juu na baadaye kushawishi wengine nao wawe na tabia hizo pia.

Chukua mfano wa uongo au ufisadi wa wanasiasa, chanzo ni jamii nzima kukumbatia uongo na ufisadi na kuchukulia kama kitu cha kawaida. Watu wanaweza kuonekana wakikemea na kulaani, lakini wape nafasi ndogo tu na watajinufaisha wao kuliko wengine.

Hivyo kabla hatujawalalamikia viongozi au watu maarufu kwa tabia fulani walizonazo, tusisahau kwamba watu hao wametoka ndani ya jamii tuliyopo hivyo tabia hizo ni uwakilishi kutoka kwenye jamii.

Kila aliye nafasi ya juu kwenye jamii yoyote ile, amejengwa na jamii hiyo na sifa alizonazo ndizo zinazokubalika na jamii nzima, kama ingekuwa kinyume na hapo, mtu huyo asingepata nafasi.

Na unaweza kusema kwamba walio maarufu au wenye madaraka wana nguvu ya kuamua watakavyo, lakini nguvu hiyo haipo kwenye mikono yao, bali ipo kwenye mikono ya wale walio chini yao. Hakuna kiongozi au mtu yeyote maarufu anaweza kufanya chochote kile kwa nguvu zake mwenyewe, bali anatumia nguvu za wengine kutekeleza yale anayotaka.

Njia sahihi ya kubadili na kuboresha jamii yoyote ile ni kukazana kujenga utamaduni mpya, inachukua muda na kazi, lakini baada ya muda, jamii itajenga sifa mpya na wanaokuwa maarufu au kupata uongozi wanakuwa na sifa hizo.

Chukua mfano kwenye uvutaji wa sigara, kuna kipindi uvutaji wa sigara ulionekana kama jambo la kifahari na wengi walivuta, tena hadharani. Lakini kampeni za kupunguza uvutaji wa sigara zilipopamba moto, utamaduni ukabadilika, uvutaji wa sigara haukuonekana tena jambo la kifahari, badala yake jambo la aibu. Na kwenye jamii nyingi zilizostaarabika, mtu akitaka kuvuta sigara, anaenda kujificha kabisa.

Kila mmoja wetu ana mchango wa kujenga utamaduni mpya, kwa kuanzia kwenye familia zetu, kazi zetu na biashara zetu. Hatua unazoweza kuchukua kwenye ngazi hizo ndogo, zitakuwa na mchango mkubwa kwenye kujenga jamii iliyo bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha