Kwenye kila jamii, huwa kuna mtu au watu ambao hutengwa kwa ajili ya kutupiwa lawama pale mambo yanapokuwa hayaendi vizuri.

Hilo halijaanza leo, limekuwepo yangu enzi na enzi, ni watu wakutupiwa lawama ndiyo wamekuwa wanabadilika.

Kuna kipindi kuwatafuta wachawi na kuwachoma ilikuwa kitu maarufu, pale jamii ilipopata majanga, wengi waliamini kuna wachawi ambao wamesababisha hilo na baadhi ya watu walishutumiwa na kuhukumiwa bila hata ya ushahidi.

Kwenye jamii nyingine waliozaliwa na vilema waliokuwa wa kulaumiwa na kutolewa kafara ili kuondokana na majanga mbalimbali.

Na kwa zama hizi, viongozi na wale waliofanikiwa wamekuwa ndiyo watu wa kutupiwa lawama kwenye mengi yanayotokea kwenye maisha ya wengi.

Kunapokuwa na changamoto au tatizo lolote, huwa kuna vitu vingi vinavyochangia, vitu ambavyo ni vigumu kwa mtu wa kawaida kuweza kuvielewa.

Kwa kuwa wengi hawana muda na wala hawataki kujiumbua kujua yale yaliyochangia kwenye matatizo mbalimbali, huwa wanafurahi pale wanapopata mtu wa kumlaumu kwa matatizo yao.

Sisi hatupaswi kuingia kwenye mkumbo huo, tunapaswa kujua chanzo halisi cha kila tatizo ili kuweza kulitatua. Kupata mtu wa kulaumu kunaweza kutupa raha ya muda mfupi, lakini hakuondoi tatizo husika.

Usifuate mkumbo wa watu wanaolaumu mtu au kitu fulani kama ndiyo chanzo cha matatizo yao, jua mambo ni magumu kuliko wao wanavyoyarahisisha na kama unataka kuupata ukweli na kutatua hali hiyo lazima uweke juhudi za ziada.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha