Mimi huwa siyo msikilizaji wa redio au mfuatiliaji wa habari au mitandao ya kijamii kwa namna yoyote ile.
Ila siku za karibuni nimejikuta kwenye mazingira ambayo unakuwa na watu wengine wanaosikiliza redio na hivyo sikuwa na njia ya kukwepa hilo.
Nilishangazwa sana na vitu ambavyo vilikuwa vinapewa uzito kwenye karibu kila stesheni ya redio, nilifikiri labda mimi ni mgeni hapa duniani.
Msisitizo mkubwa ulikuwa huu ni mwezi (Februari) wa wapendanao na kilele ni tarehe 14. Kila kipindi kiligusia hilo, kila wakati watu walikumbushwa kuhusu siku hiyo na kuulizwa wamejiandaaje.
Yaani kwa nilichojifunza kwa siku chache, kama mtu anasikiliza redio hizo kila siku, lazima akili yake italaghaiwa na siku hiyo utachukuliwa kama sikukuu kubwa ya kitaifa inayohitaji hata watu wawe na mapumziko.
Lakini kupenda kwangu kudadisi kulinifanya niendelee kujiuliza kwa nini hilo liko hivyo na niliona ni njia nzuri ya kuwaandaa watu kwa ajili ya kuwapa matangazo mbalimbali. Kwani kila biashara ilikuwa inatumia mwezi na siku hiyo kuwafanya watu washawishike kununua wanachouza.
Sasa hiyo ni kwa redio tu, bado tv, magazeti, mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano.
Kikubwa nilichojifunza tangu nimeacha kufuatilia habari mpaka sasa ni kwamba asilimia zaidi ya 90 ya habari na mawasiliano mengine ya mitandaoni siyo ukweli.
Bali ni vitu unavyoweza kugawa kwenye makundi matatu;
Kundi la kwanza ni kiki, hapa ni pale watu wanapotaka wazungumziwe na watu kwa sababu wanataka umaarufu. Wasanii na hata baadhi ya viongozi wamekuwa wanatumia vyombo vya habari na mitandao kwa hili, kusema au kufanya mambo yatakayowafanya watu wawazungumzie zaidi.
Kundi la pili ni propaganda, hizi ni taarifa zisizo za kweli wala sahihi, lakini zinazotolewa kwa lengo la kubadili mtazamo na mwelekeo wa watu. Kikundi cha watu wenye nia fulani ya kujinufaisha, huwa kinaendesha propaganda za kuwasukuma wengine kuamini na kuchukua hatua fulani zenye manufaa kwa wanaoendesha propaganda hizo.
Kundi la tatu ni wahamisha mada, hawa ni wale wanaokuja na mada mpya kuwaondoa watu kwenye mjadala wa zamani ambao unawaathiri watu hao. Labda kuna kitu wananchi wanakitaka kutoka kwa Serikali, mjadala umekuwa mkali, ghafla inakuja mada nyingine ambayo inawafanya wananchi waachane na mada ya mwanzo na hivyo serikali kupata ahueni.
Vyombo vyote vya habari, mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano, vimekuwa vinatumika sana katika kusambaza mambo hayo matatu. Wanaoyasambaza wanataka wewe uamini ni ukweli, lakini kwa uhalisia siyo ukweli na hawataki ujue hilo.
Ndiyo maana nimekuwa nakushauri uachane na vitu hivyo kabisa, kwa sababu hakuna utakachokosa na utapata utulivu mkubwa, kwa sababu husumbuliwi na yeyote anayetaka kukushawishi au kukubadili kwa namna fulani.
Unajikuta ukiwa na utulivu mkubwa, wakati kila mtu anataharuki kutokana na yale anayolishwa kwa njia mbalimbali.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Asante kocha,mimi kwangu sina redio wala Tv mpaka mtu akija huwa anashangaa navyoishi na uwezo wa kumiliki ninao.Yahani kiki,propaganda na wahamisha mada vinateka sana watu haswa ushabiki wa mpira nakisiasa ambapo mwisho wa siku hakuna unchoondoka nacho kwa faida kwa maisha yako,zaidi ya kuzidi kuendelea kubishana tuu.Ila kwa muda huo mchache umeona jinsi watu wanavyotekwa na kuteswa nateknolojia hizo.
LikeLike
Nina system kwa ajili ya muziki, kuwasikiliza baadhi ya wanenaji, vitabu…… Lakini sifungulii radio. TV ni size ya screen ya laptop, ninatazama citizen ya Kenya kipindi chao kimoja SHAMBA SHAPEUP ninapata maarifa mengi ya kilimo na ufugaji. Vituo vya TV tz niliacha kuvifuatilia. Havielimishi kilimo au ufugaji bali siasa…..sijui nani kafungua nini…kawatembelea wakulima gani, kawaahidi nini! Niliacha.
LikeLike
safi sana mzee Mbise
LikeLike
Asante Mbise kwa kutushirikisha hili muhimu kwenye kujifunza.
LikeLike
Asante Hendry kwa nyongeza hii ya mfano halisia kwako.
LikeLike