Utulivu wa akili, yaani ile hali ya kutokuwa na wasiwasi au mashaka juu ya maamuzi uliyofanya ni kitu chenye gharama.
Je wewe unaijua gharama ya utulivu wa akili yako na kuwa tayari kuilipa ili uondoke kwenye wasiwasi na msongo?
Chukua mfano huu, unataka kununua simu ya aina fulani, kwenye duka ambalo linauza simu za uhakika, bei ni laki tatu. Kabla hujanunua, mtu wa karibu kwako anakuambia yeye alinunua simu hiyo hiyo yenye viwango hivyo hivyo kwa laki mbili.
Unavutiwa na hilo, unaona kuna uwezekano wa kuokoa laki nzima. Unamwambia akuelekeze aliponunua simu yake ili na wewe ukaipate kwa gharama ya chini. Anakuelekeza, ni sehemu ya mbali na uchochoroni ambapo kufika unapotea mara kadhaa.
Unafika na kupata simu kwa bei rahisi, unashukuru kwa kuwa umeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha. Unawaambia wakupe risiti, wanakujibu hawawezi kutoa risiti au hata wakikupa basi hawataandika kiasi cha fedha ulicholipia.
Lengo lako ni simu, na umeshaiona, hivyo unakubali uuziwe bila risiti halisi. Unachukua simu na kuiwasha, iko vizuri kabisa. Unaondoka nayo na kufika nyumbani, katika kuitumia unagundua ina matatizo fulani.
Unapanga kurudi kwenye duka ulilonunua, wanakuambia uiache simu na kwenda kuichukua baada ya siku mbili. Siku mbili unaenda, simu bado haijatengamaa, wanakuambia rudi baada ya siku tatu. Unazunguka hapo kwa zaidi ya wiki mbili, unaipata simu, lakini bado haifanyi vizuri kama ulivyotegemea.
Wakati unaipata simu kwa bei rahisi uliona umeokoa kiasi kikubwa cha fedha, lakini baadaye umekuja kukilipa kiasi hicho na hata ziada kupitia mahangaiko ya kuikamilisha simu hiyo.
Kama ungenunua kwenye duka la uhakika ambapo unalipa fedha kubwa, hata ungepata tatizo, usingezungushwa kama ilivyotokea kwenye duka lisilo la uhakika.
Hiyo ndiyo dhana ya gharama ya utulivu wa akili, kuna mambo unaweza kuyafanya ukiona unaokoa gharama, lakini ukajikuta unazilipa gharama hizo kwa kukosa utulivu wa akili, kwa kusumbuka kuliko ungefanya bila kuhangaika na kuokoa muda.
Kila unapofanya maamuzi yoyote, siyo ya fedha pekee, iangalie sana dhana ya utulivu wa akili. Usiangalie kila kitu kikienda kama ulivyopanga, badala yake angalia kama vitu vitakwenda tofauti na hapo pata picha ni wasiwasi na msongo kiasi gani utaupata katika hilo.
Ni bora ulipe gharama kubwa zaidi kupata utulivu wa akili, kuliko uokoe gharama na uje kuzilipa kwenye mahangaiko ya akili, kwa wasiwasi na msongo.
Vitu vinavyouzwa kwa bei kubwa ambapo kuna vya aina hiyo vya bei ndogo, kuna sababu ya kutofautiana huko kwa bei, kwenye bei kubwa utapata utulivu wa akili, kwenye bei ndogo utapata msongo, wasiwasi na hofu iwapo mambo yatakwenda tofauti na ulivyotegemea.
Ni muhimu kujua uko tayari kulipa kiasi gani cha ziada ili kupata utulivu wako wa akili na hivyo unapokutana na kitu kinachotofautiana bei, chukua cha bei juu ili kupata utulivu wa akili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hii dhana iko sahihi sana, iliwahi kunitokea mara kadhaa. Niliapa sitanunua tena kifaa cha kielectronic Kariakoo.
LikeLike
Asante Sebastian kwa kutushirikisha uzoefu wako kwenye hili.
Muhimu ni kununua sehemu inayoaminika, ambapo bei itakuwa kubwa, lakini utakuwa na utulivu wa akili.
LikeLike