Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Why don’t we learn from history? Kilichoandikwa na B. H. Liddell Hart.

Kitabu hiki ni mkusanyiko wa mafunzo ambayo B. H. Liddell Hart aliyekuwa mwanajeshi na mwanahistoria alikuwa ameyaandaa na baadaye kuchapwa na mtoto wake anayeitwa Adrian J. Liddell Hart

Sir Basil Henry Liddell Hart (31 October 1895 – 29 January 1970), alikuwa kapteni wa jeshi la Uingereza na mwanahistoria wa kijeshi. Aliandika vitabu mbalimbali vya mbinu za kivita na kuonesha makosa ambayo yamekuwa yakifanywa kwenye vita na kuleta madhara makubwa.

Mafunzo yake ya kivita yalikuwa yakitumiwa na majeshi ya nchi mbalimbali kipindi cha vita ya kwanza na ya pili ya dunia.

Kitabu kina sehemu tatu, historia na ukweli, serikali na uhuru na vita na amani. Uchambuzi utakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza itakuwa na uchambuzi wa sehemu mbili za kwanza za kitabu na sehemu ya pili itakuwa na uchambuzi wa sehemu ya tatu na hitimisho.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, tujifunze jinsi ambavyo serikali, majeshi na hata watu binafsi tumekuwa tunarudia makosa kutokana na kutokujifunza kutoka kwenye historia.

Utangulizi kutoka kwa mwandishi.

Kuandika kuhusu historia ni kazi ngumu na inayochosha sana. Hiyo ni kwa sababu kuujua ukweli inahitaji mtu kuweka kazi ya ziada.

Historia imetawaliwa na uongo ambapo waandishi na wanahistoria wengi hulazimika kuandika kisichokuwa kweli hasa maisha yao yanapotegemea kuwaridhisha wengine.

Inahitaji mtu kuwa na uhuru wa kipato kwenye maisha ili uweze kuutafuta ukweli na kuandika kilicho kweli bila ya kushinikizwa na yeyote.

Uandishi wa historia unahitaji muda na uvumilivu kwani unapogusa kitu kimoja, unagundua kimeungana na vitu vingine vingi, ambavyo vyote unapaswa kuvichunguza kwa undani ili kujua ukweli wake.

Pamoja na ugumu wa kuandika kuhusu historia, kuna manufaa yake ambayo ni kama ifuatavyo;

1. Ni kitu kinachompa mtu hamasa kadiri anavyoendelea kuchunguza na kujifunza.

2. Ni kazi inayoipa akili mazoezi na hivyo kuizuia isizeeke haraka.

3. Ni kazi ambayo manufaa yake yanadumu kwa muda mrefu.

Historia siyo tu muhimu kwa mataifa, bali pia ni muhimu kwa mtu mmoja mmoja kwani inatusaidia kujijengea falsafa binafsi na kutuzuia kurudia makosa ya wengine huku ikitusaidia kuwa na hekima.

Mwanahistoria wa kale, Polybius, amewahi kusema kwamba njia bora ya kujifunza ni kupitia makosa na majanga yanayowakumba wengine.

Historia inatupa nafasi ya kujifunza hayo na kutupa matumaini kwamba hata mambo yawe magumu kiasi gani, huwa yana mwisho, baada ya giza nene ni mwangaza.

Historia ina manufaa makubwa kwa mtu mmoja mmoja, kwa taifa na dunia kwa ujumla. Kama tunataka kuwa na maisha bora, kuepuka kurudia makosa waliyofanya wengine na kuwa na matumaini wakati tunapitia magumu, tunapaswa kujifunza kutoka kwenye historia.

Thamani ya historia.

Lengo kuu la historia ni ukweli, kujua nini kilitokea na kwa nini kilitokea. Kwa maneno mengine, lengo la historia ni kujua uhusiano na visababishi vya matukio mbalimbali.

Ili historia iwe sahihi na yenye manufaa, lazima isimame kwenye ukweli, kitu ambacho kinahitaji kazi na maadili kukisimamia. Watu wengi hawapendi ukweli, kwa sababu huwa haubembelezi au kutekeleza matakwa yao binafsi.

Historia ina ukomo wake, japo inaweza kutuonesha uelekeo, haiwezi kutupa maelezo kuhusu hali ya njia itakavyokuwa. Lakini ukomo huu haufanyi historia isiwe muhimu, bali unakuwa ni tahadhari ambayo mtu anapaswa kuwa nayo anapojifunza kupitia historia.

Historia inatuonesha nini tunachopaswa kuepuka, hata kama haiwezi kutufundisha kipi cha kufanya, itatuonesha makosa yaliyofanywa na wengine ili tusiyarudie.

Bismarck amewahi kunukuliwa akisema; “wapumbavu husema wanajifunza kwa uzoefu, napendelea kujifunza kupitia uzoefu wa wengine.” Ni kupitia historia ndiyo tunaweza kujifunza kupitia uzoefu wa wengine, kuangalia makosa waliyofanya ili tusiyarudie na kukosea kama wao.

Jamii nyingi zimekuwa zinachukulia umri wa mtu kama kipimo cha hekima, kwamba mwenye umri mkubwa ana uzoefu mkubwa na hivyo kuwa na hekima zaidi. Lakini ukiangalia kupitia historia, hilo haliwezi kuwa kweli, mwenye umri mkubwa ambaye anatumia uzoefu wake binafsi, hawezi kuwa na hekima ukilinganisha na mwenye umri mdogo anayejifunza kwenye historia.

Kama mtu ana miaka 80 na anatumia uzoefu wake binafsi, atazidiwa na mwenye miaka 40 ambaye amejifunza historia ya miaka elfu 3 iliyopita. Uzoefu binafsi pekee hautoshi, historia ina mengi ya kujifunza ambayo mtu mmoja hawezi kuyapitia yote kwa uzoefu wake mwenyewe.

Mwandishi anasema kama mtu anajua kusoma na kuandika, ni uzembe kama akili yake haina miaka zaidi ya elfu tatu.

Ni Polybius aliyesema kuna njia mbili za kuijenga jamii, ya kwanza kupitia makosa yake yenyewe na ya pili kupitia makosa ya wengine. Njia ya kwanza ni ngumu na yenye maumivu, njia ya pili ni rahisi na isiyoumiza. Maarifa ambayo mtu anayapata kwa kujifunza kupitia historia ni maarifa bora kwenye maisha.

Historia ni kumbukumbu za hatua na makosa ya mwanadamu. Inatuonesha kwamba hatua huwa zinapigwa taratibu lakini makosa yanatokea haraka. Inatupa fursa ya kujifunza na kunufaika kwa makosa ya waliotutangulia.

Wengi hufanya makosa na kuchukulia historia kama somo linalowahusu wanahistoria pekee, lakini historia ni kitu kinachogusa kila sehemu ya maisha yetu na hivyo inamhusu kila mtu. Kwa taaluma na tasnia yoyote ile, kuna watu waliotangulia ambao walifanya makosa mbalimbali, kujifunza kupitia wao inatuzuia tusirudie makosa yao.

Mbinu za kisayansi.

Kuweza kukabiliana na changamoto na matatizo ya dunia, kuweza kuyaona jinsi yalivyo, kuyachambua na kufikia ukweli, mbinu za kisayansi zinahitajika.

Hapo mtu anapaswa kuachana na upendeleo alionao na kuwa tayari kudadisi na kuhoji kila kitu badala ya kukipokea kilivyo.

Lazima mtu awe tayari kujikosoa yeye mwenyewe na kujisukuma kuutafuta ukweli badala ya kuchukulia mazoea.

Lengo la kwanza kwenye historia linapaswa kuwa ukweli na njia ya kufikia ukweli huo ni kutumia mbinu za kisayansi.

Pale mtu anaposikia chochote kinachopingana naye au kukosoa anachosimamia, hapaswi kukikataa kwanza, bali anapaswa kujiuliza swali hili; je ni kweli? Swali hilo linamsukuma kuchimba ili kujua ukweli, kwa kuweka upendeleo wake pembeni na kulikabili jambo kama ni jipya kwake.

Mtu hapaswi kupinga au kukataa wazo kwa sababu ya sifa za mtu aliyetoa wazo hilo au kukubaliana na kitu kwa sababu kimetolewa na wenye mamlaka. Bali mtu anapaswa kufanya uchunguzi kujua kama kitu ni kweli, maana ukweli huwa upo wazi pale njia sahihi zinapofuatwa.

Kama mtu anakubaliana na kitu kwa sababu tu hakipaswi kuhojiwa, mtu huyo anakuwa amekubali kwamba kitu hicho siyo kweli. Ukweli huwa hauhitaji kulindwa wala kutetewa, ukweli huwa upo wazi na ukichunguzwa unabaki kuwa ukweli. Lakini uongo unajua ukichunguzwa utajulikana, hivyo nguvu kubwa hutumika kuulinda ili usihojiwe au kuchunguzwa.

Hatua ya kwanza ya kuufikia ukweli ni kuwa na mashaka kwa kila jambo ambalo hujathibitisha ukweli wake. Mafunzo ya Chang-Tsai yanaeleza: “Kama unaweza kuwa na mashaka pale wengine wanapokuwa na uhakika, unakuwa kwenye nafasi ya kupiga hatua.

Kuhofia ukweli.

Tunajifunza kwenye historia kwamba kwenye kila zama, watu wengi huwa wanakuwa upande usio wa ukweli. Wengi hupokea kile wanachoambiwa na mamlaka bila ya kukihoji, kwa sababu mamlaka huwa zinapenda utii wa watu na kama watu wakijua ukweli, hawatakuwa na utii ambao mamlaka hizo zinataka.

Tunajifunza zaidi kwenye historia kwamba pale ukweli unapofichwa, matokeo yanayopatikana huwa siyo mazuri. Madhara yote makubwa ambayo yametokea duniani, yalianza na kufichwa kwa ukweli.

Pale baadhi ya vitu vinapochukuliwa kama ni vitakatifu na mwiko kuhojiwa, ndipo uongo hupata nafasi ya kukua na kuleta madhara makubwa. Ukweli huwa hauogopi kuhojiwa au kuchunguzwa.

Watu wengi huwa wanahofia ukweli kwa sababu wanajua unavuruga uhakika ambao tayari wamejijengea, hivyo huendelea kujilisha na kuamini uongo ili kutotikisa kile ambacho wamekiamini maisha yao yote.

Njia ya uhakika ya kuyafanya maisha kuwa bora ni mtu kuyakabili maisha kwa kufungua macho yake na kuutafuta ukweli, badala ya kuyaendea maisha kama kipofu au mlevi.

Ni mara chache sana utakutana na mtu ambaye swali lake la kwanza kwa kila anachokabiliana nacho ni; je ni kweli? Kama swali hilo halijawa sehemu ya mtu, ni dhahiri ukweli siyo kipaumbele kwa mtu huyo na kupiga hatua itakuwa vigumu kwake.

Hatari kubwa kwenye maisha ni pale historia inapopindishwa na ukweli kufichwa ili kuwapa watu matumaini fulani. Ni kosa linaloleta madhara makubwa lakini limekuwa linarudiwa kila mara.

Serikali au taasisi kwa nia njema zinaweza kuchagua kuficha ukweli fulani ili kuzuia wananchi wasitaharuki na kukata tamaa, lakini hilo huwa linaleta madhara makubwa kutokana na ukweli unaofichwa.

Ukweli haupaswi kufichwa kwa namna yoyote ile, ukweli unapaswa kuwa wazi kwa sababu ndiyo njia pekee ya watu kuwa huru.

Mwenendo wa udikteta.

Tunajifunza kutoka kwenye historia kwamba madikteta huwa wanafuata mwenendo unaofanana.

Katika kuingia kwenye madaraka;

1. Huonesha utawala uliopo au uliokuwepo kabla yao haukuwa mzuri au kutengeneza uhasama baina ya makundi ya watu.

2. Huahidi mambo makubwa na yasiyo na ukomo, ambayo huwa hawawezi kuja kuyatimiza.

3. Hudai kwamba wanataka madaraka kamili na yasiyohojiwa (absolute power) kwa kipindi kifupi, ili kuinyoosha nchi, lakini wakishayapata madaraka hayo huwa hawayaachii.

4. Huwa wanatengeneza hali ya wananchi kuwaonea huruma kwa kutengeneza njama feki dhidi yake na hivyo kutaka apate madaraka zaidi. Hutaka watu wawaonee huruma kwa kuwa wanajitoa kwa ajili yao na kujitoa kwao kunawaweka kwenye hatari.

Katika kubaki kwenye madaraka.

1. Huanza kuwaondoa wale waliowasaidia kuingia madarakani na kuonesha kwamba ni wasaliti.

2. Hukandamiza ukosoaji na kuwaadhibu wale wote wanaozipinga au kuzikosoa sera zao, hata kama wanachosema ni kweli.

3. Huweka dini upande wao na kuhakikisha viongozi wa dini wanakuwa watiifu kwao na inaposhindikana kwa dini zilizopo huwa tayari kuchochea kuanzishwa kwa dini mpya zinazotimiza matakwa yao.

4. Huwa wanatumia fedha za umma kwenye miradi mikubwa na inayoonekana na kujisifia wameleta maendeleo kama fidia ya uhuru ambao wanakuwa wameupora kwa umma.

5. Huwa wanaichezea sarafu na kufanya uchumi wa nchi uonekane unakua vizuri tofauti na uhalisia.

6. Huwa wanaanzisha vita au uadui na mataifa mengine au kukuza migogoro fulani kama njia ya kuwafanya watu wasione uhalisia wa mambo yanayoendelea ndani. Hutumia njia hiyo kuhamisha hasira za wananchi kutoka kwenye uongozi wake na kwenda kwenye adui aliyetengenezwa.

7. Husisitiza sana kuhusu uzalendo na kuutumia huo kama njia ya kuwafanya watu kuwa watiifu kwake, wale wanaompinga wanaonekana siyo wazalendo.

8. Hujijengea umaarufu binafsi na kufanya yale yanayowafurahisha watu ili tu kuendelea kubaki kwenye madaraka, kitu kinachopelekea kwenye anguko lao.

Mwenendo huu umekuwa unarudiwa tangu enzi na enzi na bado watu wamekuwa hawajifunzi mapema na kuchukua hatua sahihi.

Mienendo isiyo sahihi.

Pamoja na maendeleo makubwa ambayo dunia imepiga, hasa kwenye mfumo wa demokrasia, kumekuwa na mienendo isiyo sahihi ambayo mwandishi alikuwa anaiona katika kipindi chake. Mienendo hiyo mpaka sasa ipo na imekuwa siyo kiashiria kizuri.

1. Urasimu umekuwa mkubwa kitu kinachochelewesha kufikiwa kwa maamuzi mbalimbali.

2. Baadhi ya viongozi wamekuwa wanajijengea sifa binafsi na kuzitumia kuminya demokrasia.

3. Chaguzi nyingi zimekuwa siyo huru na za haki kama demokrasia inavyotaka.

4. Propaganda zimekuwa ni nyingi katika kuwashawishi wananchi kukubaliana na vitu fulani, wao wanaona ni maamuzi yao kumbe wameathiriwa na propaganda.

5. Udhibiti wa usambaaji wa maarifa na taarifa umekuwa mkubwa kitu kinachohatarisha upatikanaji wa ukweli.

Mfumo wa demokrasia unapaswa kulindwa na kila mtu kwa sababu ni rahisi watu kuutumia vibaya na kutekeleza maslahi yao na hata kubadili mfumo na kuwa wa kidikteta.

Viashiria vya hayo ni vingi kwa zama tunazoishi sasa.

Rafiki, karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu hiki ambao unatuonesha jinsi ambavyo hatujifunzi kutoka kwenye historia na hivyo kurudia makosa yale yale.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na vingine jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Karibu pia upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.