Nimewahi kukutana na ujumbe huu mtandaoni ambao ulinifikirisha sana, ujumbe unasema; kama uko njia panda kati ya kunichagua mimi au kumchagua mtu mwingine, usinichague mimi.

Huo ni ujumbe mfupi na mzito sana ambao unahitaji muda uweze kuuelewa vizuri. Lakini ujumbe mkubwa uliopo ndani yake ni kwamba kama inabidi umchague mtu mmoja kati ya wawili na kama unajikuta njia panda, maana yake huwajui vizuri watu hao wawili au huwaamini vya kutosha.

Kwani ukiwa unamjua mtu na ukiwa unamwamini, huwezi kuwa njia panda katika kumchagua.

Kadhalika kwenye maamuzi yetu mbalimbali, kama kila unapofika kwenye kuamua unajikuta njia panda, maana yake hujui kwa kina kile unachopaswa kuamua au hujui unakosimamia.

Unapokuwa na misingi unayoiamini na kuisimamia, maamuzi hayapaswi kuwa magumu, kwa sababu vitu vinakuwa wazi. Ndiyo maamuzi yataumiza, lakini utajua umeyafanya kwa msingi gani.

Unapokuwa huna msingi na unapokuwa unataka kuwaridhisha au kuwafurahisha wote wanaohusika ndiyo unajikuta ukiwa njia panda na kushindwa kufanya maamuzi.

Jijengee msimamo na misingi unayoitumia kwenye maisha yako, unapofika kwenye maamuzi usibahatishe, rudi kwenye misingi yako na fanya maamuzi mara moja.

Mfano kama moja ya misingi yako ni kwamba huamini kwenye njia za mkato za kufanikiwa, huhitaji muda mrefu kuamua kuhusu fursa unayoletewa kwamba unaweka pesa na kuja kuvuna mara mbili ndani ya muda mfupi. Tayari hilo liko kinyume na misingi yako, halihitaji hata mjadala.

Ila unapokuwa huna misingi, huna unachosimamia, utaanza kuchukua muda kupitia kwa kina, utaanza kusikiliza maoni ya wengi na wengi watakushawishi na kukuponza kuingia kwenye fursa hiyo na kuishia kupoteza.

Kuwa na misingi na misimamo kunasaidia sana kufikia maamuzi sahihi kwa haraka. Kama unakwama kwenye maamuzi, unachokosa ni misingi na msimamo. Jijenge kwenye hilo ili uokoe muda wako na kufanya yenye manufaa kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha