Kupenda unachofanya ni kitu ambacho kimekuwa kinashauriwa sana kama mtu anataka kufanikiwa kwenye jambo lolote lile.

Lakini ushauri huo haumaanishi kwamba hutaumia kwenye kukifanya, utaumia sana, ila kwa kuwa unakipenda, utayavumilia mateso unayokutana nayo.

Mafanikio makubwa yanahitaji gharama kubwa, gharama ambayo kama huna msukumo mkubwa kutoka ndani yako, hutaweza kuilipa.

Mafanikio hayaji kwa kufanya nusu nusu, yanahitaji kujitoa kweli kweli kitu ambacho kinawezekana kama tu unapenda mno kile unachofanya au pale unapokuwa huna mbadala mwingine.

Kuna watu watakuambia unaweza kufanya kwa muda, au unaweza kufanya pale unapojisikia, lakini hiyo siyo kweli. Ingekuwa rahisi hivyo kila mtu angekuwa amefanikiwa.

Mafanikio ni machache kwa sababu ya gharama kubwa inayohitajika kulipwa, ambayo wengi hawana ujasiri na utayari wa kuilipa.

Wengi hawajajitoa kweli kwenye kile wanachotaka, ndiyo maana huhangaika na kila kinachokuja mbele yao.

Wengi wana mengi mbadala ya kufanya kiasi kwamba wakikutana na ugumu kwenye moja wanaliacha na kwenda kwenye jingine.

Kinachohitajika ni mtu kupenda mno kile unachotaka kufanikiwa, kiasi kwamba huna muda wa kuhangaika na mengine.

Inabidi ukipende kama mtu aliyeingiwa na pepo au mzimu fulani kwenye kitu hicho na huoni kingine chochote.

Mafanikio ni kazi iliyokamilika, iliyo ngumu na isiyo na mwisho, kama hupendi kweli kila unachopenda au kama hujakichagua kwamba ndiyo pekee, hutaweza kupambana mpaka kufanikiwa na kuendelea kubaki kwenye mafanikio.

Hivyo unaposikia watu wanasema unapaswa kupenda unachofanya hawamaanishi kwamba itakuwa rahisi, bali wanamaanisha unapaswa kuwa tayari kupambana na kila ugumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha