2272; Kama hutaki matusi yakuumize…
Kama matusi ya wengine yakuumize, usikubali pia sifa wanazokupa zikuvimbishe kichwa.
Mara nyingi watu wanapotusifia na kutuambia maneno mazuri tunafurahi na kujisikia vizuri.
Lakini watu wanapotutukana au kutukosoa tunachukia na kujisikia vibaya.
Hali zote tunazitengeneza sisi wenyewe na wala siyo maneno wanayotoa wengine.
Unapofurahishwa na sifa zao, jua kabisa unajiandaa kuumizwa na matusi au ukosoaji wao.
Wale wale wanaokusifia huwa ndiyo wa kwanza kukukosoa na kukutukana na ndiyo maana huwa inauma sana.
Kwa kuwa huwezi kuwapangia watu waseme nini juu yako, njia sahihi ya kupokea kila wanachosema watu ni kutokujali, kutokuweka sana moyoni.
Watu wamekusifia, waambie asante kisha songa mbele, usiyape uzito sana maneno yao.
Na pale watu hao hao watakapokukosoa au kukutukana, haitakuumiza sana maana hukuweka uzito kwenye sifa, matusi hayatakuwa na nguvu kwako.
Wajibu wako ni kufanya kilicho sahihi mara zote, na kujitathmini kwa kila unachofanya.
Unapogundua umekosea, kupitia kujitathmini mwenyewe au kwa wengine wanavyokuambia, jirekebishe kwa kuchukua hatua sahihi.
Kama hujakosea, endelea kusimama kwenye njia sahihi na kufanya kilicho sahihi.
Iwe watu wanakusifia au kukukosoa, swali muhimu kujiuliza ni je unachofanya ni sahihi?
Swali hilo litakusaidia kuliko kuhangaika na sifa au ukosoaji ambao watu wanakupa.
Ukiweza kufaulu kwenye hili la kutokujali, unakuwa umefikia uhuru wa juu kabisa kwenye maisha yako.
Hata inapokuja kwenye maumivu, uchovu na mengine, kama kinyume cha hayo hakikufurahishi, basi hayo hayawezi kukuumiza.
Unapoteza uhuru wako pale unaporuhusu watu au hali fulani ndiyo ziamue ujisikie vizuri au vibaya.
Wewe kuwa juu ya hilo, onesha kutokujali kwenye kujisikia vizuri au vibaya na mara zote fanya kilicho sahihi, maisha yako yatakuwa tulivu na yenye uhuru na mafanikio makubwa.
Kocha.
asante kocha
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike