2316; Mchango Wako Ni Kupitia Kazi Yako…

Kila mtu ana ndoto ya kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi kwake na kwa watu wengine.

Kila mtu anapenda kuwasaidia wale wenye uhitaji kwenye maisha.

Lakini wengi huvurugwa katika kutekeleza mipango hiyo.
Wengi huhangaika na mambo yasiyo sahihi katika kutimiza malengo yao.

Chukua mfano wa mtu anayetaka kuwasaidia sana wenye uhitaji, anaamua kwenda walipo na kuwasaidia kazi zao mbalimbali, mfano kuwapikia au kuwafulia.

Unaweza kuona umetoa mchango mzuri kwa watu hao, lakini ni mchango usio na ufanisi.
Kwa wewe kwenda kuwasaidia moja kwa moja inagusa wachache.
Lakini kama ungetumia muda na nguvu hizo kuweka kwenye kazi yako, ukaongeza zaidi kipato chako na kisha ukachangia fedha kwenye mashirika yanayotoa misaada, utakuwa umefanya kwa ukubwa zaidi.

Njia ya wewe kuibadili dunia, njia ya wewe kuacha alama ni kupitia kazi/biashara yako uliyochagua kufanya.
Usihangaike na mambo mengine, hata yaonekane ni mazuri kiasi gani, ufanisi wake siyo mzuri kama ukifanya kupitia kazi au biashara yako.

Kazi au biashara yako ndiyo njia ya wewe kupata fedha na ukishazipata kwa wingi utaweza kuwasaidia wengi utakavyo.
Weka umakini wako kwenye maeneo sahihi kwako.

Kocha.