Mawazo 10 ya kuingiza fedha kupitia simu yako.

Kama unatumia simu janja (smartphone) na una mtandao wa intanetu, una fursa nyingi za kuingiza kipato.

Hapa kuna mawazo kumi unayoweza kutumia kuingiza fedha kwa simu yako.

  1. Fursa ya kujifunza zaidi. Kujifunza na kubobea kwenye chochote unachofanya ni njia ya uhakika ya kuongeza kipato.
    Unaweza kujifunza kwa kusoma vitabu, kusikiliza na kuangalia mafunzo mbalimbali. Pia unaweza kujiunga na kozi mbalimbali na kusoma kupitia simu yako.

  2. Kuandika na kuuza kazi zako za uandishi kwa njia mbalimbali. Kupitia simu yako unaweza kuandika makala, vitabu na hata kuandaa mafunzo ya sauti na video na kuyauza kwa njia mbalimbali.
    Vitabu unaweza kuuza kwa nakala tete, makala kwa watu wenye mitandao inayolipa au watu kukulipa ili wasome makala.

  3. Kuendesha kundi la mafunzo na ushauri.
    Kwa kutumia simu yako unaweza kuanzisha kundi la wasap, telegram au mitandao mingine na watu wakajiunga kwa kulipa ada.
    Kwa kuwa kwenye kundi hilo watu wanakulipa ada na wanapata nafasi ya kupata mafunzo unayotoa na ushauri wa mambo mbalimbali.
    Chagua eneo ambalo watu huwa wanakuomba sana ushauri kisha geuza kuwa kundi utakaloweka wenye uhitaji huo. Pale mtu anapokuomba ushauri kwenye eneo hilo, mwalike ajiunge kwenye kundi lako.

  4. Kuanzisha na kuendesha blogu.
    Kupitia simu yako unaweza kuanzisha na kuendesha blogu ambayo utaitumia kuingiza kipato kwa njia mbalimbali.
    Kupitia blogu unaweza kuuza bidhaa na huduma zako na pia unaweza kuweka ada ya watu kulipa ili wasome.
    Jukwaa zuri la kutumia kwenye blog ni WordPress.

  5. Kuendesha mtandao wa barua pepe za kulipia (newsletter)
    Mtandao wa substack umeboresha mfumo wa kutoa maudhui mbalimbali kwa kutumia barua pepe. Kupitia simu yako unaweza kuanzisha mtandao wako wa barua pepe, ukawaandikisha watu na wakakulipa kusoma.
    Uzuri wa substack ni unaweza kuendesha mtandao wako kwa watu wanaosoma bure na wanaosoma kwa kulipia, hivyo inakuwa rahisi kuwashawishi wanaosoma bure walipie.

  6. Kuuza vitu ulivyonavyo au biashara yako.
    Kuna mitandao mbalimbali ya mtu kujiunga na kuuza vitu vyako mfano kupatana.
    Kwa kuwa na simu, unaweza kupiga picha kitu unachouza na kuweka kwenye mitandao hiyo.
    Inaweza kuwa kitu ulichonacho ambacho kwa sasa hukitumii tena. Au inaweza kuwa bidhaa za biashara uliyonayo.

  7. Kufanya masoko.
    Kwa kutumia simu yako unaweza kutangaza na kutafuta masoko kwa biashara unayofanya au biashara ya wengine.
    Hapa pia unaweza kuendesha kurasa za kibiashara za mitandao ya kijamii kwa ajili ya biashara yako au biashara za wengine.

  8. Kufundisha.
    Unawez kutumia simu yako kufundisha madarasa mbalimbali ya mtandaoni. Unaweza kuendesha tuisheni kwa njia ya simu. Pia kuna mitandao kama smartclass ambayo inatoa fursa kwa walimu kufundisha mtandaoni na kuingiza kipato.

  9. Huduma shirikishi.
    Kuna biashara mbalimbali zinaendeshwa kwa mfumo wa uchumi shirikishi (shared economy) kama Uber, Airbnb, Bolt n.k.
    Kwa kutumia simu yako na kuwa na chombo cha usafiri unaweza kuongeza kipato chako.

  10. Kuwa msaidizi wa mbali.
    Kuna watu mbalimbali ambao wanapenda kusaidiwa majukumu mbalimbali ambayo hawawezi au hawana muda wa kuyafanya. Mfano uhariri wa nyaraka mbalimbali, upangiliaji wa vitu na kukusanya taarifa mbalimbali.
    Kwa kutumia simu yako, unaweza kuwa msaidizi wa watu kwenye majukumu unayoweza vizuri, wakawa wanakutumia, unayafanyia kazi kisha wanakulipa.

Nyongeza; Kufuatilia matumizi yako.
Watu wengi huwa hawajui matumizi yao ya siku ni kiasi gani. Na kutokujua kunakuwa chanzo kikubwa kwao kuwa na matumizi yaliyopitiliza.
Kwa kutumia simu yako unaweza kuweka app ambayo itakusaidia kufuatilia matumizi yako na hilo litakupa mwanga wapi fedha zako zinapotelea ili uweze kuziokoa.
Kama utaokoa fedha unazopoteza ni sehemu ya kuongeza kipato pia.

Mawazo haya kumi yanaweza kuingiza kipato kwa yeyote anayeweza kuweka juhudi.
Kama una simu, mtandao wa intaneti na muda wa angalau saa moja kila siku unaweza kuchagua wazo lolote hapo na kuanza kulifanyia kazi.

Kama utachagua wazo lolote kati ya hayo, karibu tujadiliane zaidi ili uweze kulitekeleza kwa ufanisi mzuri.

Kocha.