2335; Shamba lisilolimwa…

Shamba lenye rutuba nzuri lakini halijalimwa, huwa halipotezi rutuba yake. Bali rutuba hubaki pale ikiwa imelala.

Shamba hilo litaota magugu lakini nayo hayawezi kumaliza rutuba kubwa ya shamba.

Siku akitokea mtu na kuona fursa nzuri iliyo kwenye shamba hilo na kuanza kulilima, ananufaika sana.

Hivyo pia ndivyo binadamu tulivyo.
Kila binadamu ana uwezo mkubwa sana ndani yake.
Uwezo ambao hauwezi kuharibiwa kwa namna yoyote ile.

Kama uwezo huo hautumiki, unakuwa umelala ndani ya mtu.
Atahangaika maisha yake yote kufanya mambo yasiyo na tija huku uwezo mkubwa ukiwa umelala ndani yake.

Ni mpaka siku moja mtu huyo anapoamka kutoka kwenye usingizi na kusukumwa kutumia uwezo ulio ndani yake.
Ghafla anajishangaa akiweza kufanya makubwa ambayo awali alidhani hawezi.

Tukiendelea na mfano huo wa shamba, nataka nikupe takwimu ambazo zitakushtua kidogo.

Kama uwezo wako ni shamba lenye rutuba nzuri la ukubwa wa heka kumi, kwa sasa unalima heka moja tu.
Yaani yote uliyoweka kufikia mpaka sasa, unatumia moja ya kumi tu ya uwezo mkubwa ulio ndani yako.

Hebu fikiria ukitumia tatu ya 10 au hata tano ya 10, utafanya miujiza mikubwa kabisa kwenye maisha yako na kuzalisha matokeo ambayo hawajawahi kuonekana.

Kwa bahati mbaya sana, ulipozaliwa hukuja na kitabu cha maelezo kuhusu wewe. Ukienda kununua hata simu, unapewa kitabu cha maelezo ya jinsi ya kutumia simu hiyo na uwezo wake.

Lakini wewe hukuja na kitabu chochote kinachoelezea uwezo wako na jinsi unavyoweza kutumika kwa usahihi hapa duniani.
Huo ni mtego unaopaswa kuutegua, hilo ni fumbo la kutatua kwenye maisha yako.

Wachache wanaotatua hilo wanafanya makubwa na kufanikiwa sana. Wengi wanaoshindwa kutatua hilo wanakufa na rutuba kubwa ndani yao ikiwa haijatokea.

Je wewe utakufa na rutuba yako ikiwa haijatumika au utapambana kuitumia kabla hujafa?
Hilo ni swali unaloweza kujibu mwenyewe, hakuna anayeweza kukusaidia.

Kocha.