2351; Laini, Ngumu Na Imara…

Nassim Taleb kwenye kitabu chake cha Antifragile anaeleza mifumo yote inaweza kuwa kwenye kundi moja kati ya haya matatu.

Kundi la kwanza ni laini (fragile), hii huwa rahisi kuvunjika pale inapokubwa na tatizo. Mifumo laini huwa haiwezi kuhimili matatizo na changamoto mbalimbali.
Mifumo hii inaweza kuonekana ni mizuri pale mambo yanapokuwa rahisi. Ni mpaka mambo yawe magumu ndiyo udhaifu wa mifumo hiyo unaonekana wazi.

Kundi la pili ni ngumu (resilient), hii ni mifumo inayokuwa migumu kiasi cha kuweza kuhimili matatizo na changamoto mbalimbali. Mifumo hii huwa ni migumu na haibadiliki, japo inaweza kuonekana ni mizuri, ina udhaifu mkubwa wa kuweza kuvunjwa na matatizo makubwa au yanayojirudia rudia.
Kama tunavyojua, hata tone la maji linalojirudia rudia linaweza kuvunja mwamba mgumu.

Kundi la tatu ni imara (antifragile), hii ni mifumo ambayo inazidi kuwa bora kadiri inavyokutana na magumu na changamoto mbalimbali. Mifumo hii haibaki kama ilivyo, bali inakuwa bora zaidi kiasi kwamba hata tatizo au changamoto ikijirudia haiwezi kuivunja mifumo hiyo.
Mifumo imara inazidi kuwa bora kadiri inavyokumbana na changamoto au magumu mbalimbali.

Unachohitaji kwenye maisha ni kujenga mifumo imara, ambayo inazidi kuwa bora kadiri unavyokwenda.
Kwa sababu unajua magumu na changamoto zitaendelea kuwepo, njia pekee ya kuendelea vizuri ni kuwa na mifumo imara.

Ni rahisi kujenga mifumo hii kwa kujifanyia tathmini kwa kila tatizo au changamoto unayokabiliana nayo, ili kuhakikisha haiwezi kukirudia tena.

Mfano kama umekuwa na changamoto za kifedha na madeni ni kwa sababu mfumo wako wa fedha ni laini, tatizo kidogo linavunja mfumo huo. Njia ya kuufanya mfumo huo kuwa imara ni kuwa na akiba ya dharura kiasi kwamba tatizo likitokea halikuangushi kabisa.

Kadhalika kwenye afya, mahusiano, kazi na hata biashara. Angalia mifumo uliyonayo kwenye kila eneo la maisha na itengeneze kwa namna ambayo unapokutana na magumu au changamoto, unabaki ukiwa bora kuliko ulivyokuwa awali.

Tuchukue mfano huu rahisi kabisa;
Umefukuzwa kazi ghafla na unajikuta huna hata fedha za kuendesha maisha yako, maisha yanabadilika na kuwa hovyo, mfumo wako ni laini.

Umefukuzwa kazi ila una akiba ya kuweza kuendesha maisha yako kwa miezi sita ijayo. Mfumo wako ni mgunu, utakuwezesha kujipanga katika hicho kipindi, lakini kikiisha hujapata kazi au kipato kingine, mfumo unavunjika.

Umefukuzwa kazi ila tayari ulikuwa na biashara yako ya pembeni unayoiendesha ukiwa kwenye ajira. Kitendo cha kufukuzwa kazi kinakufanya ukaweke nguvu zaidi kwenye biashara yako ya pembeni, unaikuza kiasi cha kutohitaji kutafuta tena kazi, hapa mfumo wako ni imara.

Huu ni mfano unaolenga eneo moja, unaweza kuangalia maeneo mengine katika makundi hayo matatu.
Lengo ni kuwa kwenye kundi la tatu.

Kocha.