2396; Mambo ya kufanya unapokuwa chini kabisa…
Safari ya maisha siyo barabara iliyonyooka.
Ni njia yenye vilima, mabonde na kona nyingi.
Kuna kupanda na kushuka, kwenda mbele na kurudi nyuma.
Kila mtu anayapitia haya kwenye maisha kwa wakati wake na kwa viwango vinavyotofautiana.
Mambo yanapokuwa mazuri, huwa tunajisahau na kudhani yataenda hivyo wakati wote.
Na mambo yanapokuwa magumu huwa tunakata tamaa na kuona hatuwezi kusimama tena.
Kila siku giza linapoingia, huhofii kwamba kutakuwa na giza milele. Unakwenda kulala ukiwa na uhakika kwamba kesho kutakucha tena.
Wakati wa kiangazi kukali hukati tamaa na kuona ndiyo mwisho, unajua masika yanakuja.
Hivyo pia ndivyo unapaswa kuyachukulia maisha yako, kujua hali yoyote unayopitia sasa siyo ya kudumu, bali ni ya muda tu.
Hapa tutakwenda kuangalia mambo makubwa matatu ya kufanya pale unapokuwa chini kabisa ili maisha yako yaendelee kwenda vizuri.
Kwanza kabisa jua uvumilivu ndiyo utakaokuvusha, haijalishi unapitia magumu kiasi gani, kamwe usikubali kukata tamaa.
Endelea kuwa na imani kwamba huo ni wakati tu na utapita.
Uvumilivu ndiyo unakuweka kwa muda mrefu zaidi mpaka ukutane na fursa ambazo ni nzuri.
Pili tengeneza utaratibu wako wa siku ambao utauishi kila siku bila kuacha hata siku moja.
Hata kama unaona kabisa kwamba dunia imefika mwisho, wewe fuata utaratibu wako wa siku.
Vitu vya kuweka kwenye utaratibu wako wa siku;
1. Kuamka mapema kabla jua halijachomoza.
2. Kusali na/au kutahajudi.
3. Kusoma kitabu angalau kurasa 10.
4. Kuyaandika malengo na ndoto zako kubwa.
5. Kufanya mazoezi ya mwili.
6. Kuandika vitu vitabo unavyoshukuru kuwa navyo kwenye maisha.
7. Kuwasiliana na watu wa katibu.
8. Kujifunza kitu kipya.
9. Kujaribu kitu kipya.
10. Kuongeza thamani kwa mtu mwingine.
Tatu tafuta vitu vinavyokuweka bize na kukuchosha siku nzima. Kadiri unavyokuwa na muda mwingi ambao huna cha kufanya, ndivyo unavyopata muda wa kutengeneza fikra za hofu ambazo zinazidi kukudidimiza.
Usijiruhusu kuwa na muda mtupu, jaza siku yako nzima na shughuli mbalimbali zinazokuweka bize na kukuchosha kwelikweli. Yaani mpaka muda wa kulala unapofika, unakuwa umechoka kiasi cha unapoingia kitandani usingizi unakuchukua mara moja.
Kuwa na muda mwingi ambao huna cha kufanya, ni hatari kwako unapokuwa chini. Huo muda utautumia kutengeneza mabaya yatakayokuudidimiza zaidi.
Nyongeza; epuka habari, mitandao ya kijamii na kufuatilia maisha ya wengine unapokuwa chini. Ni rahisi kujilinganisha na wengine na kuzidi kujididimiza.
Waepuke pia wale ambao wana mtazamo hasi, ambao muda wote wanaongea jinsi mambo ni mabaya na yatazidi kuwa mabaya.
Tayari mambo ni mabaya kwako, huhitaji tena kuendelea kusikia habari hizo. Unachohitaji sana ni namna ya kuvuka hali unayopitia.
Zingatia haya unapokuwa chini ili uweze kuvuka kipindi hicho salama na kurudi juu.
Kwenye ukurasa wa 2397 tutaangalia mambo ya kufanya unapokuwa juu ili unaposhuka chini usianguke vibaya.
Kocha.