Rafiki yangu mpendwa,
Siku za karibuni yalitokea machafuko nchini Afrika Kusini ambapo wananchi walifanya maandamano yaliyoambatana na uporaji kwenye maduka mbalimbali.

Hapa sitaeleza sababu ya maandamano hayo, bali nitaeleza kitu kimoja kilichoishangaza dunia kuhusu hayo maandamano.

Waandamanaji walivamia maduka makubwa na kupora kila aina ya bidhaa. Kuanzia vyakula, vinywaji, mavazi na vifaa vya kielektroniki kama tv, simu na vingine.
Wengine walionekana wakiwa wamebeba wanyama kama mbuzi, kuku na hata nguruwe.

Waandamanaji walionekana kuwa na hasira na kueleza sababu ya uporaji wao ni kukosekana kwa usawa baina ya wananchi.
Kwamba wachache wana maisha mazuri huku wengi wakiwa na maisha magumu.

Hilo nalo sitalielezea zaidi kwa sababu lengo langu hapa ni kukuonyesha kitu ambacho waandamanaji hao hawakukiiba, ambacho kingeweza kuyabadili maisha yao kwa kiwango kikubwa sana.

Kitu hicho ni vitabu.
Katika maduka yote makubwa ambayo waandamanaji walivunja na kupora, hakuna duka la vitabu hata moja ambalo lilivunjwa.
Hata pale ambapo duka la vitabu lilikuwa ndani ya duka jingine kubwa, waliiba vitu vingine vyote lakini hawakugusa kabisa vitabu.

Hicho ndiyo kitu cha kushangaza mno kuhusu waandamanaji hao.
Maana wameiba vitu ambavyo havidumu na kuacha kile ambacho wangeiba kingedumu sana kwao.

Kuna pande mbili za kuliangalia hili, ambazo zote zina funzo kubwa kwetu.
Upande wa kwanza ni waandamanaji hawajui thamani ya vitabu na ndiyo maana hawajahangaika navyo. Hapa tunajifunza umuhimu wa kuthamini vitu ambavyo vina matokeo ya muda mrefu.

Upande wa pili ni waandamanaji siyo wasomaji wa vitabu na ndiyo maana waliiba kila kitu isipokuwa vitau. Hapa tunajifunza umuhimu wa kusoma vitabu, kwani unayabadili kabisa maisha yako.

Rafiki, nimekuwa nasema mara kwa mara kwamba kitu pekee unachoweza kuiba kwa wengine na kikawa na manufaa makubwa kwako ni vitabu.
Vitabu vina siri kubwa za mafanikio, vina nguvu ya kuyabadili maisha yako kabisa na maarifa yake yanadumu milele.

Ukiina fedha utazitumia na zitaisha.
Ukiiba chakula utakula na utasikia tena njaa.
Ukiiba simu utaitumia na itapitwa na muda wake au kuharibika.
Lakini ukiiba maarifa, yatadumu na wewe milele.

Kama umejifunza kitu na kikabadili mtazamo wako, utabaki na mtazamo huo mpya kwa maisha yako yote.
Kama ulikuwa unaamini kuna vitu huwezi, lakini ukajifunza kwenye vitabu kwamba unaweza na ukajaribu ukaweza, hilo litadumu na wewe mpaka unakufa.

Hivyo basi rafiki yangu, kama unapata nafasi ya kuiba chochote, iba maarifa. Pata na usome vitabu ambavyo vitaifungua kabisa dunia yako, vitabadili mtazamo wako na kukuwezesha kuona yake ambayo huoni sasa.

Somo kubwa tunalojifunza kwa waandamanaji wa Afrika Kusini kupitia uporaji wao ni kuacha kuhangaika na vitu visivyodumu na kuchagua kuhangaika na vile vinavyoweza kudumu kwenye maisha yako.

Wapi unaweza kuiba vitabu?

Sijaandika hapa kukupa tiketi ya kwenda kuvunja maduka ya vitabu na kuiba vitabu, hilo ni koda kisheria.
Lakini tunaishi kwenye zama za taarifa, ambapo mtandao wa intaneti umerahisisha sana upatikanaji wa vitabu bure kabisa.

Hapa kuna sehemu tatu nakuelekeza ambapo unaweza kwenda kuiba kitabu chochote unachotaka.

Moja ni mtandao wa Library Genesis ambao unapatikana kwa anwani; http://libgen.rs/ ingia na tafuta kitabu unachotaka.

Mbili ni mtandao wa Z Library ambao unapatikana kwa anwani; https://b-ok.africa/ ingia na tafuta kitabu unachotaka.

Tatu ni channel ya SOMA VITABU TANZANIA ambapo unapata vitabu na chambuzi zake, anwani yake ni; https://t.me/somavitabutanzania
Kama unasema kiingereza ni kikwazo kwako, basi kwenye channel hiyo unapata chambuzi za vitabu kwa lugha rahisi kabisa ya Kiswahili.
Lakini pia unapata nafasi ya kushiriki mijadala ya moja kwa moja ya vitabu kila wiki.

Rafiki, iba kile chenye manufaa ya kudumu kwako, ambacho ukikipata na kukitumia, utaweza kupata kwa wingi vile ambavyo wengine wanahangaika kuiba kila siku.
Vitabu ni hazina kubwa kwa mafanikio yako. Karibu tusome na kujadiliana pamoja maarifa ya vitabuni na jinsi tunavyoweza kuyatumia ili kuyaboresha maisha yetu.

Kupata vitabu vizuri vya Kiswahili vilivyochapwa fungua; https://somavitabu.co.tz/
Kupata vitabu vizuri vya Kiswahili vya nakala tete fungua; www.bit.ly/somavitabuapp

Nina ombi moja kwako rafiki yangu, naomba uwashirikishe wengine ujumbe huu muhimu ili uwasaidie kupata mwanga wa kuyapata maarifa yatakayobadili maisha yao. Watumie wengi uwezavyo na utakuwa umechangia katika kuwasaidia watu kuyabadili maisha yao.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.

Ndani yako una nguvu ya kutenda miujiza mikubwa, nguvu ambayo ukiijua na kuitumia hutahitaji hata kuiba, kwani utaweza kufanya mengi unayotaka. Pata kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA leo kwa kuwasiliana na 0752 977 170.