2401; Hisia, Hadithi, Mantiki…

Hivyo ni vitu vitatu tunavyotumia katika kufanya maamuzi yote kwenye maisha yetu.

Huwa tunadhani tunafanya maamuzi kwa mantiki, kisha kuyajengea hadithi na kuwa na hisia nayo.

Lakini sivyo tunavyofanya.
Huwa tunafanya maamuzi kwa hisia kwanza, kisha tunatengeneza hadithi inayotetea maamuzi hayo na mwisho ndiyo tunatafuta mantiki ya kutetea maamuzi yetu.

Unaweza kudhani wewe ni tofauti, lakini unajidanganya tu, huna nguvu ya kwenda kinyume na mtiririko huo.

Kwa kujua hili unaweza kulitumia kwa namna mbili;

Moja ni kuhakikisha muda wote unakuwa kwenye hisia nzuri kwako kuweza kufanya maamuzi bora.
Kuwa na hisia chanya za upendo, matumaini, furaha, na shauku kubwa.
Epuka hisia za hofu, wivu, chuki na kukata tamaa.

Mbili ni unapotaka kuwashawishi wengine wafanye maamuzi ya aina fulani, usihangaike na mantiki, wewe hangaika na hisia.
Angalia namna unaweza kugusa hisia zao kwa namna ambayo itawasukuma kufanya maamuzi unayotaka wafanye.

Sisi binadamu ni viumbe wa hisia ambao huwa tunahalalisha maamuzi yetu kwa mantiki.
Ukiweza kudhibiti hisia zako, umeweza kudhibiti maisha yako.

Kocha.