2402; Kuna watu watakuona takataka…

Kitu kimoja muhimu sana unachopaswa kukijua kwenye safari yako ya mafanikio, na ambacho kitapunguza sana makali ya safari hiyo kwako ni hiki; haijalishi unafanya nini, kuna watu watakuona wewe ni takataka kabisa.

Wataona ni mtu usiyefaa na dunia ingekuwa bora kama usingekuwepo kabisa.
Kwa kuwa una msukumo mkubwa ndani yako wa kufanikiwa na kwa kuwa hujali kingine chochote isipokuwa mafanikio yapo, kuna watu watachagua kukuchukia.

Watu hao watakuwa wanaomba kimoyomoyo ukutane na mabaya na pale mabaya yanapokukumba watafurahi sana.

Unaweza kuumizwa na hili, hasa pale wanaofanya hivi wanapokuwa watu wa karibu kwako, watu ambao ukifanikiwa watanufaika pia.

Lakini kuumizwa na hilo ni kupoteza muda na nguvu zako kwenye mambo yaliyo nje ya uwezo wako.

Falsafa ya Ustoa inatuasa kujua mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu na yale yaliyo nje, kisha kuhangaika na yaliyo ndani ya uwezo wetu na kuachana na yale yaliyo nje ya uwezo wetu.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako, kilicho ndani ya uwezo wako ni wewe kuishi maisha ya kweli kwako, kujitambua, kujua kusudi lako kubwa na kuwa na ndoto kubwa unazofanyia kazi.

Kilicho nje ya uwezo wako ni kutaka kila mtu akukubali na akupende.

Ukitumia nguvu na muda kuhangaika na yaliyo nje ya uwezo wako, hutayafanikisha, lakini pia utakosa muda wa kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wako.

Ishi maisha ya kweli kwako, fanya kile chenye manufaa kwako na kwa wengine na usisumbuke kwa sababu kuna watu wanakuona takataka.
Hayo ni matatizo yao binafsi, usiruhusu yakusumbue.

Kocha.