Rafiki yangu mpendwa,
Kama umekuwa unasoma kazi zangu kwa muda, unaujua msimamo wangu kuhusu usomaji wa vitabu.
Ninaamini kutoka ndani yangu na bila shaka yoyote kwamba mtu asiyesoma vitabu, hajui anachofanya kwenye maisha, anaishi kwa kubahatisha tu.
Na kama mtu anaishi kwa kubahatisha hawezi kufika kwenye mafanikio makubwa.
Haya siyo mapya, bali ndivyo ilivyo tangu enzi na enzi, wale wanaosoma vitabu wamekuwa wanapata fursa nzuri ambazo wale wasiosoma hawazipati.
Na kama ambavyo Mark Twain amewahi kusema, mtu anayejua kusoma ila hasomi vitabu, hana tofauti na asiyejua kusoma. Maana wote wanakosa vitu vizuri.
Hivyo bila ya ubishi wowote, usomaji wa vitabu ni hitaji la msingi kabisa la maisha ya mafanikio.
Lakini pamoja na manufaa makubwa tunayoyapata kwenye vitabu, kuna baadhi ya vitu huwezi kuvipata kupitia usomaji pekee.
Kuna vitu unajifunza na kuelewa vizuri pale unapokuwa kwenye eneo la tukio, ukiwa umezungukwa na wengine wanaojifunza kama wewe.

Sehemu ambayo unaweza kujifunza yale ambayo huyapati kwenye vitabu ni kwenye semina ya kukutana ana kwa ana.
Yafuatayo ni mambo kumi ambayo unayapata kwa kushiriki semina ambayo huwezi kupata kupitia usomaji pekee.
1. Kujenga mtandao wako.
Unaposhiriki kwenye semina, unajenga na kukuza mtandao wako wa mafanikio.
Kwani ni kwenye semina pekee ndipo unakutana na watu wenye mtazamo kama wako.
Huwa tunalalamika jamii zetu hazina watu wengi wenye mtazamo wa mafanikio.
Unapohudhuria semina za mafanikio, unakutana na watu sahihi wa kuambatana nao.
2. Kubadili mazingira.
Unaposhiriki semina, unayabadili mazingira yako. Unapata nafasi ya kujifunza ukiwa kwenye mazingira ambayo ni tofauti na ulivyozoea.
Wakati mwingine unalazimika kusafiri na hilo linakuweka kwenye mazingira mapya zaidi.
Kwa kujifunza kwenye mazingira ya tofauti, unakumbuka kwa muda mrefu zaidi.
3. Kujifunza bila usumbufu.
Unapokuwa unasoma kitabu, au kusikiliza kitabu kilichosomwa au kuangalia video, usumbufu ni rahisi kuondoa umakini wako.
Ni rahisi kuahirisha na kujiambia utaendelea baadaye, kitu ambacho huwa hakitokei.
Umapokuwa kwenye semina, usumbufu haukuondoi kwenye kujifunza.
Utakaa mpaka semina iishe na hivyo utajifunza yale yote yaliyopo.
Linaweza kua tukio la mara moja, ila ukaondoka na mengi kuliko unavyosoma vitabu vingi.
4. Kujifunza kwa vitendo.
Katika kujifunza, huwa kuna hatua mbalimbali unapewa za kuchukua. Ukiwa unajisomea mwemyewe, unajiambia utachukua hatua hizo baadaye. Lakini unajua vizuri kuhusu baadaye, huwa haifiki.
Unapokuwa kwenye semina, hatua za kuchukua unachukua hapo hapo, hakuna baadaye.
Kwenye semina unakuwa na fursa ya kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko kujisomea mwenyewe.
5. Kupata nguvu ya uwepo wa pamoja.
Kuna nguvu fulani huwa unaipata pale unapokuwa katikati ya kundi la watu ambapo mnafanya kitu kwa pamoja.
Ni kama ilivyo kwenye dini, biblia unayo nyumbani, na kuisoma unajua, lakini unapoenda kanisani, kuna upako wa tofauti unaupata.
Kadhalika kwenye mafanikio, unapohudhuria semina kuna upako unaoupata kwa kuwa kwenye eneo la tukio tofauti na ukijifunza mwenyewe.
Kitendo cha kuwa pamoja na kujifunza kinakupa nguvu kubwa ya kuelewa na hamasa ya kuchukua hatua.
6. Kujifunza kutoka kwa wengine.
Unaposhiriki semina, unakutana na wengine ambao wanakushirikisha yale wanayojua na uzoefu wao pia.
Hilo pekee lina thamani kubwa mno.
Maana unaposoma na kukutana na kitu kipya, ni rahisi kujiambia hili haliwezekani.
Lakini unapokuwa kwenye semina na kukutana na wengine ambao wamepiga hatua, unajionea wazi kwamba yale mapya unayojifunza yanawezekana.
7. Kushirikisha wengine unachojua.
Huwa kuna usemi kwamba hujakielewa kitu kama huwezi kumwelezea mtu mwingine naye akaelewa.
Ukiwa unasoma mwenyewe unaweza kudhani umeelewa, lakini ikawa sivyo, kitu ambacho unakuwa hujui.
Unaposhiriki semina, utahitajika kushirikisha wengine kile unachojua au uzoefu ulionao.
Hilo litakuonyesha ni kwa kiasi gani unajua na kukusukuma ujifunze kwa kina na uelewe zaidi.
Kuhitajika kuwashirikisha wengine unachojua, kunakusukuma uelewe zaidi.
8. Kupata hamasa kubwa zaidi.
Unapojisomea mwenyewe unaweza kupata hamasa.
Lakini unaposhiriki kwenye semina ya pamoja, unapata hamasa kubwa zaidi kwa sababu unakuwa umezungukwa na watu wenye mtazamo kama wako.
Hamasa unayoipata kwenye semina pia inadumu kwa muda mrefu kuliko unayoipata kwa kujisomea mwenyewe.
9. Kupata majibu ya maswali yako.
Unapokuwa unasoma kitabu na kukawa kuna kitu hujaelewa, huna nafasi ya kumuuliza mwandishi akufafanulie.
Lakini unapokuwa kwenye semina na mnenaji akasema kitu ambacho hujaelewa, unaweza kumuuliza moja kwa moja akakupa ufafanuzi.
Hivyo unaposhiriki semina, huwezi kutoka ukiwa na dukuduku lolote, unatoka ukiwa umeelewa kila kitu.
10. Kujitoa zaidi ili kupiga hatua.
Kushiriki semina kunakuingia gharama kubwa kuliko kununua kitabu au maarifa ya aina nyingine.
Kwa kuwa unafanya uwekezaji mkubwa, utajitoa na kuweka juhudi zaidi ili uwekezaji huo uweze kuwa na manufaa zaidi.
Kwa kujua kitu kimekugharimu, unakithamini na kuweka juhudi zaidi ili kukitumia kwa manufaa kwako.
Shiriki semina ili upate msukumo wa kujitoa zaidi na kufanya makubwa.
Rafiki yangu mpendwa, umejionea hapo jinsi unavyijifunza mengi na kwa kina kwa kushiriki semina kuliko kwa kujisomea vitabu pekee.
Hivyo pamoja na kusoma vitabu, shiriki semina za kimafanikio ili upate msukumo mkubwa zaidi wa kufanikiwa.
Nichukue nafasi hii kukukaribisha kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 ambayo itafanyika tarehe 16 na 17 mwezi Oktoba jijini Dodoma.
Hili ni tukio kubwa la kimafanikio linalotokea mara moja tu kwa mwaka. Kupitia semina hiyo unakwenda kupata manufaa haya kumu uliyojitunza hapa, na mengine ya ziada kama kufuatiliwa na Kocha kwa mwaka mzima.
Kama bado hujathibitisha kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021, fanya hivyo sasa ili usikose nafasi hii ya kipekee kwako.
Tuma sasa ujumbe wenye majina yako na kwamba utashiriki semina kwenda namba 0717 396 253.
Nakusubiri kwa shauku kubwa tuungane pamoja kwenye semina hii kubwa ya kimafanikio. Tuma ujumbe wako sasa ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz
