2405; Usitawanye Nguvu…
Mwanga wa jua unapotawanyika kwenye eneo kubwa, unaishia kumulika tu.
Lakini mwanga huo huo unapokusanywa eneo moja kwa kutumia lensi, unakuwa na nguvu ya kuchoma kitu na kuwasha moto kabisa.
Kuwa na mwanga wajua na lensi pekee hakutoshi, inamhitaji mtu kuweza kukusanya mwanga huo eneo moja kwa muda na siyo kuhamisha hamisha.
Hivyo pia ndivyo nguvu zetu binafsi zilivyo, tukizikusanya sehemu moja kwa muda tunaweza kufanya makubwa.
Lakini tukizitawanya, hatuwezi kufanya makubwa.
Ni dhana rahisi kuisema na kuielewa, lakini hutaona uzito wake kama huifanyii kazi.
Tayari nguvu za kufanya makubwa zipo ndani yako.
Kama hufanyi makubwa siyo kwa sababu huna nguvu za kuwezesha hilo, ila kwa sababu unazitumia nguvu hizo vibaya.
Unatawanya nguvu zako kwa mambo yasiyo na tija kwako, kitu ambacho kinakuzuia usiweze kufanya makubwa ambayo una uwezo wa kuyafanya.
Kwenye kile kipindi cha maisha yako, chagua kupaumbele chako kikuu na weka juhudi zako zote kwenye kipaumbele hicho, usitawanye nguvu zako kwenye maeneo mengine.
Kwa kila siku unayoianza, orodhesha mambo muhimu kwako kukamilisha kwenye siku hiyo na weka nguvu zako zote kwenye mambo hayo tu, usihangaike na yaliyo nje ya hayo.
Kwa kujijengea nidhamu kwenye hili, utashangaa jinsi utakavyoweza kufanya makubwa kwenye maisha yako, kwa vile ulivyo sasa.
Kuweka nguvu zako zote kwenye kitu kimoja kwa miaka mitano utazalisha matokeo makubwa kuliko kufanya kwa juu juu kwa miaka 50.
Ni kipaumbele kipi kikubwa unachokipa nguvu zako zote kwa sasa?
Kocha.