2427; Makasiriko…

Katika hali yoyote ile, aliyekasirika ndiye mwenye matatizo.

Yaani kama kuna mtu amekukasirisha, tatizo siyo mtu huyo, bali tatizo ni wewe uliyekasirika.

Kwa maana nyingine, ukikasirika maana yake una matatizo.

Na wewe angalia wazi tu ni wakati gani unakasirika.

Mara nyingi ni moja kati ya nyakati hizi tatu.

  1. Kuna mategemeo makubwa uliyokuwa nayo kwa mtu na amekuangusha kwenye mategemeo hayo.

  2. Mtu ameweza kufanya kitu ambacho wewe umeshindwa na hilo linakufanya ujione kama hufai.

  3. Umekuwa na upweke na unatamani sana wengine watambue uwepo wako, kitu unachoona kinakosekana.

Yote hayo ni matatizo yako binafsi.
1. Unapaswa kujua huwezi kuwadhibiti wengine kwa namna unavyotaka wewe, kufikiri hivyo ni kujiandaa kwa maumivu.

  1. Mwingine kufanikiwa kwenye kitu ambacho umeshindwa haimaanishi wewe hufai, ana uzoefu tofauti na wewe. Hivyo hata wewe ukijenga uzoefu huo, utaweza kufanikiwa.

  2. Usitafute kutambuliwa na wengine kwa kelele, bali fanya kitu chenye tija.

Hasira ni hisia, zinakujia ukiwa hata hujui. Kupata hisia za hasira siyo kubaya, wewe ni binadamu, ni vigumu sana umalize siku hujakwaruzana na mtu mwingine.

Ubaya ni pale unapozichochea hisia zako za hasira, ukachukua hatua kwa kuchochewa na hisia hizo na hilo kuharibu mambo zaidi.

Kila hisia za hasira zinapoingia, jiulize tatizo lako ni nini.
Utaliona wazi na kuweza kuchukua hatua sahihi ili usiendelee kuharibu zaidi.

Na mtu anapokukasirikia, jua kabisa tatizo lake ni kubwa kuliko lako.
Badala ya wewe kumkasirikia pia, muonee huruma na kwepa huo mtego.

Kocha.