Rafiki yangu mpendwa,
Ile hadithi tuliyokua tukihadithiwa kwa miaka mingi tangu utotoni mpaka shuleni imepitwa na wakati.

Hadithi kwamba nenda shule, soma kwa bidii na utapata kazi nzuri na inayolipa sana haifanyi tena kazi katika zama hizi.
Wengi wanasoma ila kazi hawapati.
Na wachache wanaozipata kazi hizo haziwalipi kama walivyotegemea.
Na bado hatari ya kupoteza kazi ni kubwa.

Hapa tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuanzisha biashara kwa mtaji kidogo baada ya kupunguzwa kazi.
Msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuomba ushauri kwenye hili alikuwa na haya ya kusema;

“Nimepunguzwa kazini nafsi yangu inakataa kuchukua hatua ya kutafuta kazi tena nahitaji kufanya biashara lakini nssf yangu ni ml 5 ninahofu nikipotea hizi nimepotea kabisa nishauri ndugu yangu nianzie wapi.” – Nelson D. R.

Nianze kwa kumpongeza mwenzetu kwa kuona njia sahihi siyo kutafuta tena kazi, bali kuanza biashara.
Wengi huwa hawafikirii hivyo, bali huendelea kutafuta kazi kitu kinachowarudisha kwenye hali waliyojikuta sasa.

Kwa kuamua kwamba biashara ndiyo kitu unakwenda kufanya, umefanya maamuzi sahihi ambayo yanaweza kukuondoa kwenye hatari ulizojikuta sasa.

Lakini changamoto kama alivyoeleza ni mtaji, kiasi cha fedha anachotegemea kupata siyo kikubwa sana, lakini ni kiasi kinachomtosha kuanza kabisa.

Kuna mambo matano muhimu ya kuzingatia katika kufanyia hili kazi.

Moja; ingia kwenye biashara ya kuuza moja kwa moja.

Kwa kuwa unaanza na mtaji kidogo, hupaswi kuingia kwenye biashara ambayo inakutaka kufanya uwekezaji wa mtaji.
Hapo utazamisha sehemu kubwa ya mtaji na ushindwe kuanza.

Hivyo ingia kwenye biashara ya kuuza moja kwa moja.
Angalia bidhaa au huduma ambayo ina uhitaji mkubwa kwa pale ulipo, kisha ingia kwenye kuiuza.
Nunua na uza kwa wateja moja kwa moja.

Hapa mwanzoni usihangaike kulipia eneo la kufanyia biashara au kuingia gharama nyingine zozote.
Wewe nunua bidhaa au huduma kisha ipeleke kwa wateja moja kwa moja.

Tumia njia mbalimbali za masoko na usambazaji ili kuwafikia wateja. Tumia matangazo ya mtandaoni, nenda nyumba kwa nyumba au ofisi kwa ofisi na tumia mawasiliano mbalimbali uliyonayo.

Lengo lako kubwa ni kuuza na kutengeneza wateja kwanza, mengine yanaweza kusubiri.
Pambana sana mwanzoni katika kutoa huduma bora kwa wateja unaoanza nao, maana hao ndiyo watakaokuletea wateja wengine zaidi.

Mbili; usitumie mtaji wote ulionao.

Kwa kuwa unaanza na mtaji mdogo, usitumie fedha yote uliyonayo kama mtaji.
Tumia kama nusu kwenye mtaji wa biashara na nusu inayobaki iweke akiba.
Kufanya hivyo kutakusaidia pale uhalisia unapokuwa tofauti na ulivyotegemea.

Huenda ulidhani biashara unayoanza nayo itatoka vizuri, unakuja kugundua uhitaji siyo mkubwa kama ulivyodhani mwanzo.
Kwa kuwa na akiba, inakusaidia kufanya mabadiliko muhimu ili biashara iendelee.

Lakini pia kuna dharura mbalimbali unaweza kukutana nazo kwenye maisha. Pale unapokuwa huna akiba yoyote, ukikutana na dharura itakutikisa sana.
Lakini ukiwa na akiba utaivuka dharura hiyo kwa utulivu mkubwa na biashara yako kuendelea.

Tatu; ifanye biashara ndiyo kila kitu kwako.

Kwa miezi sita ya mwanzo ya biashara yako, inapaswa kuwa ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako.
Punguza mambo mengine yote ambayo umekuwa unahangaika nayo na umakini wako, muda wako na nguvu zako zote peleka kwenye biashara yako changa.

Kama miezi sita ya mwanzo ya mtoto ilivyo muhimu, ndivyo pia miezi sita ya mwanzo ya biashara ilivyo muhimu.
Usipoipa biashara yako kipaumbele namba moja kipindi cha mwanzo, itaanguka vibaya.

Punguza mambo ya kijamii, mapumziko na starehe mbalimbali.
Kipindi cha mwanzo cha biashara ni vita na vita haina huruma, ni upambane upone au uzembee ufe.

Epuka sana kuhamishia tabia za kwenye ajira kwenye biashara yako mpya.
Jua kwenye biashara unahitajika masaa 24 kwa siku, siku zote 7 za wiki. Usilete mambo ya huu ni muda wa biashara na huu ni muda wangu wa mapumziko.
Biashara changa haijali hayo, kila wakati ni muda wa biashara.

Nne; punguza sana gharama za maisha.

Hatari kubwa inayoweza kukuzamisha unapoanza biashara ni gharama za maisha.
Kama gharama zako za maisha zitakuwa juu, utajikuta ukitumia fedha zaidi ya biashara ili kuendesha maisha.
Hilo litakuwa na athari kubwa kwenye biashara yako na kuizuia kukua..

Kama nilivyoeleza hapo juu, kipindi cha mwanzo cha biashara ni kipindi cha vita, hivyo pia matumizi yoyote ambayo siyo ya msingi kabisa achana nayo.
Kama siyo jambo la kufa na kupona basi linaweza kusubiri na mengi sana yanapaswa kusubiri.

Gharamia yale matumizi ya msingi na lazima tu, mengine yote achana nayo na nguvu zako zote peleka kwenye kukuza biashara yako zaidi.

Tano; jifunze na endelea kukua.

Unaanza biashara yako kidogo, lakini hupaswi kubaki kwenye huo udogo.
Unapaswa kuendea kukua kadiri muda unavyokwenda.
Ukuaji wa biashara yako unategemea sana ukuaji wako binafsi.
Kama wewe hukui, biashara yako haiwezi kukua pia.

Anza kwa kuwa  na maono makubwa kibiashara, ambayo unayafanyia kazi kila siku.
Kisha endelea kujifunza kuhusu biashara na maendeleo binafsi kadiri unavyokwenda.
Endelea kuangalia fursa zaidi za ukuaji wa biashara yako na uzitumie.
Katika kila faida unayoingiza, sehemu yake inapaswa kurudi kwenye ukuaji wa biashara.

Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA kinapaswa kuwa mwongozo wako mkuu katika kuendesha biashara yako.
Pia kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kinapaswa kuwa mwongozo wako kwenye mambo yote yanayohusu fedha.
Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170

Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kuanzisha na kukuza biashara itakayokupa uhuru na kukuondoa kwenye changamoto za kupunguzwa kazi.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz

Wasiliana na 0752 977 170 kupata vitabu.