2432; Kila kitu ni rahisi isipokuwa kufanya…
Kuahidi ni rahisi,
Kuweka malengo ni rahisi,
Kupanga ni rahisi,
Kukosoa ni rahisi,
Kuomba ushauri ni rahisi,
Kushauri ni rahisi,
Kulalamika ni rahisi.
Kila kitu ni rahisi, isipokuwa kimoja tu, ambacho ni kufanya.
Kuweka juhudi katika kufanya kitu, ili kuleta matokeo ya tofauti, ni jambo gumu mno.
Ndiyo maana kuna wafanyaji wachache sana.
Na kila anayefanikiwa huwa ni mfanyaji.
Hakuna hadithi ya mafanikio ambayo utamsikia mtu akisema kulalamika kumenifikisha kwenye mafanikio haya makubwa.
Kwa bahati mbaya ni kufanya huwa hakuchangamani na kitu kingine chochote.
Hivyo unapomuona mtu akihangaika na mambo mengine, kwa hakika jua hafanyi.
Maana angekuwa anafanya, asingepata nafasi ya kuhangaika na mengine.
Chochote kinachokuwa rahisi kwako, ambacho hakikufikishi kule unakotaka kufika, ni usumbufu na kikwazo kwako kufika huko.
Ni lazima uwe makini sana, maana hayo rahisi yanakuzunguka na kukushawishi.
Wewe kuwa mfanyaji, kuwa mzalishaji wa thamani na waache wengine wakihangaika na yaliyo rahisi ila yasiyo na tija.
Kila unapofanya kitu, chukua sekunde chache na ujiulize kama ni rahisi au sahihi.
Unafanya kitu hicho kwa sababu ndiyo rahisi kwako kufanya au unakifanya kwa sababu ndiyo sahihi kwako kufanya?
Tayari unajua rahisi na sahihi haviwezi kwenda pamoja.
Unahitaji kuchagua kimoja, kilicho rahisi kufanya ambacho hakina tija. Au kilicho sahihi kufanya ambacho hakitakuwa rahisi.
Maisha yako ni matokeo ya machaguo ya aina hiyo kila siku.
Kila unachofanya unachagua kwa namna hiyo.
Cha kushangaza sasa, kadiri unavyochagua kufanya yaliyo rahisi, ndivyo maisha yako yanavyokuwa magumu.
Na kadiri unavyochagua kufanya yaliyo sahihi, ndivyo maisha yako yanavyokuwa bora.
Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, jua kila unachofanya umechagua mwenyewe na matokeo unayopata sasa ni uchaguzi wako mwenyewe.
Kocha.