2434; Hadithi unayojilisha na kupima…

Kitu pekee kinachotutofautisha sisi binadamu na wanyama wengine kama mbuzi ni hadithi ambazo tunajipa.

Na hadithi hizo zinatokana na ubongo wetu wa mbele, ambao ni mkubwa na umeendelezwa ukilinganisha na wa wanyama wengine.

Wanyama wengine wanapokea na kuishi katika hali walizozaliwa nazo.

Lakini sisi binadamu tuna nguvu ya kuyabadili maisha yetu kwa kutumia nguvu iliyo kwenye ubongo wetu.

Kama ambavyo William James aliwahi kusema; ugunduzi mkubwa wa kizazi chetu ni binadamu wana uwezo wa kuyabadili maisha yao kwa kubadili mtazamo wao wa kifikra.

Na kama Earl Nightingale alivyowahi kusisitiza siri kubwa kabisa ni kwamba huwa tunakuwa kile tunachofikiri kwa muda mrefu.

Na hapo ndipo hadithi inapoingia.
Kile unachojiambia mara kwa mara, unachojilisha na kuamini ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako.

Vile ulivyo sasa ni matokeo ya hadithi ambayo umekuwa unaiishi kwenye maisha yako, ambayo umekuwa ukijilisha na unaiamini bila ya shaka.

Hivyo kama unataka kuyabadili maisha yako, anza kwa kubadili hadithi unayojiambia.
Tengeneza hadithi ya kile hasa unachotaka kwenye maisha yako na iamini kweli kweli.

Jilishe hadithi hiyo muda wote kupitia kujifunza mambo yanayoendana na kile unachotaka, kuyaandika malengo yako na kujiambia kauli chanya na zinazoendana na hadithi yako kwa muda mrefu.

Pia endelea kujipima kwa jinsi unavyokwenda kuona kama unaikaribia hadithi yako au la.

Fanyia kazi hilo na utashangaa jinsi maisha yako yatakavyobadilika kwa kiwango kikubwa, kwa kuanza tu na hadithi unayojilisha na kujipima katika kuiendea.

Kocha.