Rafiki yangu mpendwa,
Kwa zama tunazoishi sasa, biashara ndiyo njia pekee na ya uhakika ya kuingiza kipato kisichokuwa na ukomo.

Hivyo yeyote anayeyataka mafanikio makubwa, lazima apite njia ya biashara.

Ni jambo jema watu wamekuwa na mwamko wa kuingia kwenye biashara na hivyo biashara mbalimbali zimekuwa zinaanzishwa.

Lakini kuna changamoto moja kubwa, biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake.

Na sababu za hilo ni nyingi, lakini moja kubwa ni watu kuanzisha biashara bila ya kuwa na elimu sahihi ya biashara.

Wengi huanzisha biashara kwa kufuata mkumbo, wakisikia kitu fulani ni fursa au kinalipa sana, wanaingiwa na tamaa ya mafanikio ya haraka na kuingia.

Kinachotokea ndiyo hayo maanguko ya biashara ambayo yanawaacha watu wakiwa na maumivu na hasara kubwa.

Biashara zote zinazokufa huwa zinaonyesha dalili moja kubwa, faida kutokuonekana na mtaji kukata.
Mfanyabiashara anaona akiuza sana, lakini mwisho wa siku akiangalia haoni faida na mbaya zaidi mtaji unakuwa ukipungua.

Hapa tutajifunza nini kinapelekea hali hiyo na hatua za kuchukua ili kuinusuru biashara yako.

Msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili, alikuwa na haya ya kuandika;

“Nafanya biashara inatoka faida hakuna na mtaji unakata.” – Alice A. M.

Kama alivyoandika Alice, hiyo ni changamoto ambayo biashara nyingi sana zinapitia.
Mauzo yanakuwepo ila faida haionekani na mtaji unapungua.

Kwa kuwa ni jambo ambalo ni gumu kueleweka, watu wamelitafutia sababu nyepesi ya kuwaridhisha.

Yaani unawezaje kuelezea hali kwamba wateja wanakuja kwenye biashara na kununua vizuri tu, lakini mwisho wa siku unapopiga mahesabu ya biashara, huoni faida na mbaya zaidi mtaji unapungua.

Kwa kuwa watu hawana njia rahisi ya kulielewa hilo, wamekuja na jibu rahisi la chuma ulete. Kwamba kuna watu wanatumia nguvu za giza kuiba fedha kwenye biashara.

Wapo wanaoliamini hilo kabisa na hata kwenda kutafuta dawa ya kulidhibiti, lakini imekuwa haina manufaa. Bado biashara zinashindwa.

Kama unauza vizuri ila faida haionekani na mtaji unakata, sababu siyo chuma ulete, bali sababu ni hizi;

1. Matumizi ya fedha za biashara kiholela.
Huna nidhamu na fedha za biashara, unazitumia tu kadiri unavyotaka kwa sababu unaona ni zako.
Kosa kubwa sana, ukishaweka fedha kwenye biashara siyo zako tena, hiyo ni mali ya biashara.
Wewe umeikopesha biashara mtaji na unatakiwa uvune faida tu. Mtaji unapaswa kuuacha uzunguke kwenye biashara bila kuingiliwa.
Ingilia mtaji wa biashara na kwa hakika lazima biashara itashindwa.

2. Biashara haitengenezi faida.
Watu wengi hudhani kuuza sana ndiyo faida kwenye biashara.
Unaweza kuuza sana na bado biashara ikawa inapata hasara.
Mauzo ni sehemu moja, unapaswa kuondoa manunuzi na gharama ili kubaki na faida.
Kama manunuzi na gharama zipo juu, hata uuze kwa wingi kiasi gani, hupati faida.
Tena kama gharama zipo juu, kadiri unavyouza kwa wingi ndivyo unavyokata mtaji kwa sababu unakuwa unapoteza fedha nyingi zaidi.

3. Gharama za biashara na zako binafsi ziko juu.
Kama gharama za kuendesha biashara zipo juu, zinameza faida na biashara kupata hasara.
Kama gharama zako za maisha ziko juu, utachukua fedha nyingi kwenye biashara na itapata hasara.

4. Biashara haina wateja wazuri.
Wateja wazuri wa biashara ni wale ambao wamekuwa wananunua mara kwa mara na hata kuleta wateja wengine.
Wateja wasio wazuri ni wale wanaonunua mara chache na kutaka punguzo sana.
Unaokuwa unaanza biashara unapokea mteja wa kila aina, lakini kama usipoachana na wateja wasio wazuri, biashara yako itadhurika.

5. Hufuatilii namba za biashara yako kwa karibu.
Ukiwa unafuatilia namba za biashara yako kwa karibu, kila siku, kila wiki, kila mwezi na kuendelea, utaanza kuona mapema mwenendo usio sahihi na kuweza kuchukua hatua kabla madhara hayajawa makubwa.
Usipokuwa mfuatiliaji utaona mambo yanaenda vizuri tu, halafu siku moja ghafla mambo yanakuwa mabaya.
Mwanafalsafa mmoja amewahi kusema mambo huwa yanaanza kuharibika kidogo kidogo kwa muda mrefu, halafu baadaye yanakuja kuharibika ghafla kwa ukubwa.

Hatua za kuchukua ili kuinusuru biashara yako.

1. Fuatilia kwa makini namba hizi 5 muhimu za biashara yako;
✔Mtaji unaozunguka kwenye biashara, huu hakikisha huutoi kwenye biashara kwa matumizi binafsi.
✔Mauzo yaliyofanyika, pambana yawe juu.
✔Gharama za kuendesha biashara, pambana ziwe chini.
✔Faida, mauzo yakiwa juu na gharama zikiwa chini, moja kwa moja faida inakuwa juu.
✔Wateja, walionunua, wapya, wa zamani na waliofikiwa kwa njia mbalimbali za masoko.
Cheza na hizi namba kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila robo mwaka na kila mwaka.
Biashara haiwezi kufa bila ya kuanzia kwenye namba hizo tano.

2. Heshimu sana fedha za biashara.
Ukishaweka mtaji kwenye biashara, usipeleke tena mikono yako kugusa fedha hizo.
Acha mtaji uzunguke kwenye biashara.
Kama unaitegemea biashara kuendesha maisha yako binafsi basi jilipe mshahara kutoka kwenye biashara hiyo na mshahara utokane na faida.
Kama unachojilipa ni zaidi ya faida, jua wazi hapo hakuna biashara, ni swala la muda tu kabla hujafunga.

Piga 0752 977 170 kupata kitabu.

3. Pata elimu sahihi ya biashara.
Usiendeshe biashara kwa mazoea, badala yake endesha kwa utaalamu.
Pata elimu sahihi ya kuendesha biashara yako ili ujue yale muhimu kuzingatia na uyazingatie.
Pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ili ujue misingi sahihi ya kujenga kwenye biashara.
Kukipata kitabu wasiliana na 0752 977 170.

4. Kuwa na mfumo mzuri wa uwajibikaji.
Biashara kubwa huwa zinaendeshwa vizuri kwa kufuata misingi yote ya biashara kwa sababu zina mifumo ya uwajibikaji.
Biashara ndogo huwa zinaendeshwa kiholela kwa sababu mifumo ya uwajibikaji inakosekana.
Hakikisha unakuwa na mifumo ya uwajibikaji kwenye biashara yako ili usukumwe kuiendesha kwa misingi sahihi na ifanikiwe.
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuna mifumo hiyo ya uwajibikaji.
Kama bado hujawa mwanachama, wasiliana sasa na 0717 396 253.

Rafiki, yafanyie kazi haya uliyojifunza ili uweze kuanzisha, kuendesha na kukuza biashara yenye mafanikio makubwa.
Misingi ya mafanikio kwenye biashara ipo, ijue na kuifuata na biashara yako itafanikiwa.
Ila kama utachagua kuendelea na mazoea, jua hakuna namna utaweza kuinusuru biashara yako isife.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz