2446; Nia njema huishia pabaya…
Kila mtu anayefanya jambo lolote lile, huwa anakuwa na sababu za msingi kabisa za kulifanya na huwa analifanya kwa nia njema kabisa.
Hata kama kwa nje jambo hilo linaonekana ni la hovyo na la kijinga, sivyo anavyoona mfanyaji.
Yeye anakuwa amefikiri na kufanya maamuzi ambayo kwake ni sahihi na yana mantiki.
Tatizo kubwa ni kwamba wengi huwa tunafanya maamuzi kwa kujipa uhakika wa matokeo.
Kwa sababu tunataka sana kitu fulani kitokee, basi tunaona ndiyo kitakachotokea.
Hatujiandai kwa matokeo tofauti na tunayotarajia.
Na hapo ndipo njia njema inapoishia pabaya.
Kwa sababu mtu anakuwa amefanya kitu kwa nia njema, akijua matokeo mazuri yatapatikana na mambo kwenda vizuri.
Kinachotokea ni matokeo yanakuwa tofauti na matarajio na hilo linakuwa tofauti na nia aliyokuwa nayo mtu.
Hata watu wanaodanganya, huwa wanaanza kwa nia njema kabisa, wakijua mambo yataenda vizuri na uongo huo utaisha.
Lakini mambo hayaendi vizuri na hivyo inawabidi waendelee kudanganya.
Uongo ulioanza kidogo na kwa nia njema unageuka kuwa uongo mkubwa na wenye madhara.
Kwa sababu kila wakati mtu inabidi adanganye zaidi ili kuficha uongo wa awali.
Hatua ya kuchukua;
Mara zote fanya kilicho sahihi na sema ukweli. Usifanye kisichokuwa sahihi au kusema uongo hata kama ni kwa nia njema kiasi gani.
Hata kama utaona unafanya hivyo kwa muda mfupi usishawishike, jua matokeo yoyote unayodhani yatarekebisha kila kitu siyo ya uhakika.
Kilicho ndani ya uwezo wako ni kufanya kilicho sahihi, mengine yako nje ya uwezo wako, usijipe nayo uhakika.
Tafakari;
Njia ya kuelekea kuzimu huwa imepambwa na nia njema. Pale unapotaka kufanya kitu kisicho sahihi au kusema uongo kwa sababu una nia njema, jua unakwenda kutengeneza matatizo yatakayokusumbua kwa muda mrefu.
Kocha.
Ahsante Sana kocha kwa tafakari hii, Niko tayari kupokea matokeo ya tofauti lakini najua ntakuwa nimejifunza
LikeLike
Vizuri kwa maamuzi hayo.
Yasimamie.
LikeLike
Asante Sana kocha kwa tafakari hii, ni muhimu kusema ukweli na kufanya kilicho sahihi hata Kama inanigharimu?
LikeLike
Hakika
LikeLike