2455; Siyo lazima ujibu.

Matatizo na changamoto nyingi tunazopitia kwenye maisha, chimbuko lake ni midomo yetu, tunaongea wana na kuongea hovyo.

Mtu anaweza kufanya jambo, likakukera au kukuudhi, maneno yanaanza kukutoka ambayo yanazidi kuharibu kuliko kujenga.

Mtu anaweza kukujibu vibaya na wewe ukasukumwa kumjibu vibaya zaidi.

Maneno ni upepo mtupu, ambao una nguvu ya kuwasha moto lakini hayana nguvu ya kujenga kilichobomoka.

Hivyo kuwa na tahadhari sana unapotumia maneno, hasa pale unapokuwa kwenye hali ya kukwazika au kutokuelewana na wengine.

Hakuna mtu amewahi kugombana na mtu au kukuza ugomvi zaidi kwa kukaa kimya.

Na pia ukimya una nguvu kubwa, unawafanya watu washindwe kukutabiri na hivyo kukupa heshima kubwa.

Mara nyingi huwa tunakimbilia kujibu mambo ili kujifurahisha tu, kitu ambacho hakijawahi kuwa na manufaa yoyote.

Hatua ya kuchukua;
Pale unapokuwa umekwazika, kukasirika au kuwa kwenye hali ya kutokuelewana na wengine, hesabu mpaka 100 kabla hujajibu chochote.
Kama ni mawasiliano ya kuandika, andika jibu lako lakini usilitume, liweka kwa muda na uje usome tena baadaye, utagundua jinsi ambavyo halikuwa sahihi.
Unapokuwa na hisia za juu, fikra zinakwenda chini na hivyo utajibu kwa namna isiyo sahihi.
Ukijizuia kujibu mpaka hisia zitulie, utajiepusha na matatizo mengi.

Tafakari;
Hata mjinga akikaa kimya, atachukuliwa ni mtu mwerevu, lakini anapoongea anadhihirisha ujinga wake. Ukimya una nguvu kubwa sana, itumie.

Kocha.