2460; Lazima kuna mtu ataumia.

Kwenye moja ya vitabu ambavyo nimekuwa narudia kusikiliza mara kwa mara, How To Be A Billionaire, mwandishi anasema ukifanikiwa kutengeneza utajiri wa mabilioni, utakuwa pia umefanikiwa kutengeneza maadui wakubwa.

Kwa kifupi ni hakuna namna utaweza kufanikiwa bila ya kuwaumiza baadhi ya watu kwa namna fulani, kitu ambacho kitawafanya wawe maadui wakubwa kwako.

Hili ni funzo muhimu na la msingi kabisa ambalo kila anayetaka mafanikio makubwa anapaswa kulijua na kulielewa, kwamba mafanikio unayopigania yatawaumiza baadi ya watu na hilo litakutengenezea maadui.

Na maumivu tunayozungumzia hapa siyo ya kuwadhuru watu au kufanya mambo yenye madhara kwao.
Bali ni maumivu yanayotokana na wewe kuvunja mategemeo ya watu kwako.

Mfano hitaji la kwanza kwako kufanikiwa ni kusema HAPANA kwenye mambo mengi ambayo tayari unayafanya sasa, ila hayana mchango kwenye mafanikio makubwa unayotaka.

Tayari kuna watu wameshakuzoea wewe kwenye hayo unayofanya, usidhani watapokea kirahisi HAPANA yako.
Hawatakubaliana nayo na watafanya kila mbinu kuhakikisha unabaki kama ulivyo.
Kama umejitoa kweli kufanikiwa hutakubali hilo, hivyo utapambana nao kweli kweli kusimamia mabadiliko yako.

Na hapo ndipo watu wataumia, hapo ndipo utaonekana umebadilika, una dharau, hujali na maneno mengine ambayo watu watapenda kutoa kwa ajili yako.

Kibinadamu unaweza kuumizwa na hayo na kuona labda unakosea, lakini unapaswa kujua kwenye haya maisha maumivu hayakwepeki, hasa kwenye safari ya mafanikio.
Kama hautakuwa tayari kuwaumiza wengine katika kusimamia kile unachotaka, maana yake umechagua kuwa tayari kujiumiza wewe mwenyewe kwa kutokupata unachotaka.

Jua hili wazi na utakayechagua kumuumiza, asitumie kama hatia ya kukutudisha nyuma.

Hatua ya kuchukua;
Kwa mafanikio makubwa unayotaka, jua kabisa ni watu gani watakaoumizwa na mabadiliko makubwa unayoendelea kufanya kwenye maisha yako.
Na pale unaposikia vilio na malalamiko ya watu hao, furahia, maana upo kwenye njia sahihi.

Tafakari;
Mtu mmoja amewahi kusema kama unataka kupendwa na kila mtu uza pipi. Na mimi nakuambia hata ukiuza pipi bado kuna watu watachukizwa na hilo, wakisema unafaidika sana. Amua kuwagawia pipi hizo bure na kuna watu hawatapendezwa na hilo, wakisema unaozesha meno yao.
Kuishi maisha yako kutawaumiza baadhi ya watu, kubaliana na hilo.

Kocha.