2463; Kwenye muda huo huo.

Watu wamekuwa wanalalamika hawana muda wa kufanya yale wanayopaswa kufanya ili wafanikiwe.
Lakini katika muda huo huo, kuna wengi wanaofanya makubwa na kufanikiwa sana.

Nimekuwa najiuliza mara nyingi, nini kinapelekea hili? Inakuwaje kwenye muda huo huo wengine wanafanikiwa na wengine wanashindwa?

Nilielewa hilo kwa kina baada ya kusoma jibu ambalo Thomas Edison alitoa wakati anahojiwa kuhusu swala la muda.

Nitaandika kama alivyojibu;
“Kuna vitu ambavyo huwa unafanya kila siku, kila mtu anafanya hivyo. Kama unaamka saa moja asubuhi na kulala saa tano usiku, umeweka masaa 16 kwenye siku yako ambayo kuna vitu umekuwa unafanya mwenye masaa hayo kwa siku nzima. Inaweza kuwa ni kutembea, kusoma, kuandika au kufikiri. Tatizo ni kwamba watu wengi huwa wanahangaika kufanya mambo mengi kwenye muda huo, lakini mimi nafanya jambo moja tu. Kama watu watachukua muda wao wa siku na kuutumia kufanya kitu kimoja tu, lazima watafanikiwa sana. Tatizo linakuja kwamba watu wengi hawana kitu kimoja muhimu walichochagua kufanya na kupuuza vingine vyote. Mafanikio ni zao la matumizi makali ya mwili na akili.”

Sitaki kuongeza neno hapo, kila kitu kimesemwa na Edison.

Hatua ya kuchukua;
Yatafakari maisha yako, ulikotoka, ulipo sasa na unapotaka kufika. Kisha jiulize ni jambo lipi moja ambalo ukiweka juhudi kubwa kila siku litakupa mafanikio makubwa.
Jua leo ni kitu gani ambacho lazima ukipe kipaumbele kikubwa kila siku, kisha fanya hivyo.
Kwa kupeleka nguvu, akili na muda wako kwenye jambo moja, baada ya muda utapata mafanikio makubwa mno.

Tafakari;
Wanaofanikiwa na wanaoshindwa wote wana masaa 24 kwenye siku. Kinachowatofautisha ni jinsi wanavyoyatumia masaa hayo. Wanaofanikiwa wanayatumia kwenye mambo machache muhimu, huku wanaoshindwa wakiyatumia kwenye mambo mengi yasiyo muhimu.

Kocha.