2466; Unawafanyia wengine, kwa ajili yako.
Mambo mengi unayowafanyia wengine kwenye maisha, unayafanya kwa ajili yako mwenyewe.
Unawatumia hao wengine kama sababu tu, lakini mhusika mkuu ni wewe.
Chochote unachomshauri mtu mwingine, ni ushauri ambao unautoa kwa ajili yako mwenyewe. Haijalishi umeutoa kwa nani na kwa ajili ya nini, huo ndiyo ushauri ambao wewe mwenyewe unauhitaji sana kwenye maisha yako.
Kile kilichokusukuma utoe ushauri kwa ajili ya wengine, kimekufanya ujione vizuri ndani yako na kujua nini hasa unachohitaji.
Unaposema huwaamini wengine, unachomaanisha ni hujiamini wewe mwenyewe. Maana ukishajiamini wewe mwenyewe, wengine wanafikiri, kusema au kufanya nini haikubabaishi kwa namna yoyote ile. Unajiamini na unafanya mambo yako.
Lakini kama hujiamini, utaona kila mtu ni adui kwako, kila mtu anataka kujinufaisha kupitia wewe na hivyo kuona hakuna wa kuaminika.
Unapowaumiza wengine, ni kwa sababu tayari una maumivu ndani yako. Hutaki uumie mwenyewe, hivyo unahakikisha wengine nao wanaumia pia.
Unapowachukia wengine ni kwa sababu unajichukia mwenyewe. Unapowapenda ni kwa sababu unajipenda.
Hakuna chochote unachofanya kwenye maisha kwa ajili ya wengine, ambacho hakijaanzia ndani yako mwenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Chochote unachofanya kwa ajili ya wengine, jiulize ni kwa namna gani unakihitaji sana kitu hicho wewe mwenyewe.
Ushauri wowote unaowapa watu wengine, iwe wamekuomba au la, jiulize ni kwa jinsi gani wewe mwenyewe unahitaji ushauri huo, kisha anza kuufanyia kazi.
Utaweza kuwa bora sana kwenye maisha yako, kama utatumia mwenyewe yale unayofanya kwa ajili ya wengine.
Tafakari;
Ungekuwa unafanyia kazi ushauri unaowapa wengine, ungekuwa mbali zaidi ya hapo ulipo sasa. Hujachelewa, hebu anza sasa kufanyia kazi wewe mwenyewe kila ambacho unawashauri wengine, utaona mabadiliko makubwa kwako mwenyewe.
Kocha.