2472; Muda na Umakini…

Watu wengi wamekuwa wanasingizia muda kama kikwazo kwao kufanya yale yaliyo muhimu.
Wanasema hawana muda wa kufanya mambo hayo.

Mimi nimekuwa nalikataa hilo, nikisema kila mtu ana muda sawa. Hivyo ambao wanasema hawana muda, wanatafuta tu visingizio na wamekosa vipaumbele kwenye maisha yao.

Nimekuwa nawakatalia kabisa wale wanaosema hawana muda wa kusoma vitabu au kuandika. Nikieleza mbona wanapata muda wa kula na kuoga kila siku?

Lakini baada ya kuendelea kujifunza na kutafakari kwa muda, nimegundua tatizo siyo muda (time), bali tatizo ni umakini (attention). Unaweza kuwa na muda mwingi kwenye siku yako, lakini umakini ukawa mdogo.

Unaweza kuwa na masaa nane ya kufanya kazi, lakini ukawa na umakini wa masaa manne tu.
Hivyo hakuna anayekosa muda wa kufanya kitu, bali wengi wanakosa umakini wa kufanya kitu.

Na ukiangalia hilo liko dhahiri kabisa. Ni mtu gani kwenye masaa yake 24 anakosa dakika 20 za kusoma angalau kurasa 10 za kitabu kwa siku? Hayupo.
Ila nani mwenye umakini wa kutenga dakika 20 na kusoma ndipo tatizo linapoanzia.

Tunapopanga mambo ya kufanya, hatupaswi kuangalia muda pekee, badala yake tunapaswa kuangalia na umakini pia. Unaweza kutenga muda wa kufanya kitu, lakini kama hutakuwa na umakini, hutaweza kukifanya vizuri.

Angalia ni vitu gani vinahitaji umakini mkubwa kwenye kuvifanya, kisha vipe hivyo kipaumbele cha kwanza.
Vitu kama kusoma, kuandika na kufanya maamuzi muhimu vinahitaji umakini mkubwa, hivyo panga kuvifanya wakati ambao bado hujachoka.

Usihangaike na vitu vinavyohitaji umakini mdogo kabla ya kufanya vinavyohitaji umakini mkubwa.
Jua tatizo siyo muda, bali umakini. Muda unaweza kuwa nao mwingi, lakini umakini ukawa mdogo.

Hatua ya kuchukua leo;
Ni vitu gani unajua ni muhimu kwako kufanya lakini umekuwa unashindwa kuvifanya kwa sababu huna muda?
Sasa acha kuangalia muda kama kisingizio na anza kuangalia umakini. Jua ni umakini kiasi gani unahitajika kwenye kufanya vitu hivyo kisha panga kuvifanya wakati ambao una umakini mkubwa.
Tatizo la umakini haupo sawa mara zote kama muda, bali unaenda ukipungua. Fanya vile vinavyohitaji umakini mkubwa wakati umakini wako ukiwa juu.

Tafakari;
Kikwazo kwa wengi kufanikiwa siyo muda bali umakini. Wote tuna muda sawa kwenye siku zetu, lakini umakini haulingani na hata jinsi ya kutumia umakini huo haifanani.
Linda sana umakini wako, maana huo ndiyo wenye thamani kubwa kwako kufanikiwa.

Kocha.