2487; Akili na Maadili.
Tunapata shida kwenye kupata watu wa kushirikiana nao kwa sababu ya kukosekana kwa vitu hivyo viwili.
Kuna watu wanaweza kuwa na akili sana, lakini wakakosa maadili. Hawa ukiwa na mfumo mzuri ambao unazuia ukosefu wao wa maadili usiwe kikwazo, unaweza kushirikiana nao vizuri.
Kuna watu ambao hawana akili sana, ila wana maadili. Hawa ukiwapa majukumu ya kawaida wanayafanya vizuri kabisa na hawakupi usumbufu mkubwa.
Taabu ipo kwa wale ambao hawana akili na pia hawana maadili. Hawa ndiyo sumu kubwa ambao kitu kikubwa wanachoweza kufanya ni kuharibu tu.
Kwa kukosa vyote watu hao wanakuwa hatari sana, kwani wapo tayari kuharibu hata kile ambacho kinawanufaisha wao.
Kwa bahati mbaya sana, jamii yetu imejaa watu ambao hawana akili na pia hawana maadili. Ndiyo maana inakuwa vigumu sana kupata watu sahihi wa kushirikiana nao.
Hatua za kuchukua;
Katika kutafuta watu wa kushirikiana nao, angalia sana vitu hivyo viwili.
Ukipata mwenye akili na maadili hiyo ni bahati, fanya kila namna uendelee kuwa naye.
Ukipata mwenye akili ila hana maadili, hakikisha una mfumo mzuri unaoziba mianya inayoweza kutumiwa na ukosefu wale wa maadili.
Ukipata mwenye maadili ila hana akili mpangie kabisa majukumu anayopaswa kutekeleza na kumwelekeza kwa usahihi.
Ukipata ambaye hana akili na hana maadili, mwondoe haraka, ni bomu hilo.
Tafakari;
Usifanye tu kazi na kila mtu, bali weka vigezo vya wale utakaofanya nao kazi na uvifuate. Hilo litapunguza changamoto mbalimbali zinazotokana na watu.
Kocha.
Asante Sana kocha.
LikeLike
Karibu
LikeLike