2492; Kidogo kidogo halafu ghafla.

Mambo yote kwenye maisha huwa yanaanza kidogo kidogo kisha baadaye yanatokea ghafla.
Lakini mara nyingi watu huwa hawaoni yanapotokea kidogo kidogo na kuchukua hatua sahihi, wanakuja kushtuka wakati yametokea ghafla na hawawezi tena kuchukua hatua kwa haraka.

Hakuna mtu anaamka siku moja na kujikuta kwenye deni kubwa.
Huwa inaanza kidogo kidogo, deni dogo hapa, jingine pale. Inajengeka kuwa tabia ya madeni na siku moja mtu anajikuta kwenye madeni makubwa.

Biashara huwa hazifilisiki kwa ghafla tu, huwa zinaanza kidogo kidogo, kwa kupoteza fedha, gharama kubwa kubwa, faida kukosekana na wateja kupungua. Inaenda hivyo kwa muda na siku moja ghafla biashara haiwezi kujiendesha tena.

Kadhalika hata kwenye afya, hutaamka siku moja na kujikuta ukiwa na kilo 5 za ziada. Ni kitu ambacho kinaongezeka kidogo kidogo na baada ya muda unakuja kushtuka uzito ni mkubwa.

Ukiwa mtu makini na unayefuatilia kila eneo la maisha yako kwa karibu, utaona mapema mabadiliko madogo madogo kabla hayajawa makubwa.

Hatua ya kuchukua;
Kuna mambo mawili muhimu unapaswa kufanya ili kuzuia mabadiliko madogo madogo yasiwe kikwazo kwako.
Jambo la kwanza ni kujiwekea viwango vya juu kabisa ambavyo utavizingatia mara zote. Usikubali chochote chini ya viwango ulivyojiwekea. Maana unapoanza kupuuza viwango vyako, ndiyo unakaribisha matatizo makubwa baadaye.
Jambo la pili ni kujifanyia tathmini mara kwa mara, kila siku, wiki, mwezi, robo mwaka na mwaka. Tathmini hizo zinakuonyesha mabadiliko madogo madogo yanayoendelea ili uweze kuchukua hatua mapema. Kwa mfano kuona hasara kwenye biashara kwa wiki ni rahisi kuchukua hatua kuliko kuja kuiona baada ya mwaka.

Tafakari;
Palikuwa na mji mzuri, msafi na wa kupendeza sana. Baadhi ya watu wakaanza kuacha vioo vya madirisha yao vilivyopasuka bila kutengeneza. Haikuchukua muda wakaanza kutokusafisha mazingira yao. Taka zikaanza kuzagaa kila mahali na watu kutupa hovyo. Mji ukadorora, watu wengi wakauhama na ukabaki na majengo ambayo ni magofu na kuwa kitovu cha uhalifu. Hili halikuanza tu ghafla, lilianza kidogo kidogo kwa watu kutojali usafi wa nyumba zao.

Kocha.