2499; Ujuaji Mwingi.

Nikiwa shule ya sekondari, nilikuwa na biashara ya kupiga picha pale shuleni.
Siku moja walimu wakanitaka niwapige picha.
Wakati wanajipanga ili niwapige picha, mwalimu mmoja akasema angalia hiyo picha isiye ikaungua (enzi hizo tunatumia kamera za analojia).

Nilimjibu yule mwalimu mimi ni mzoefu kwenye hili zoezi la upigaji picha, siwezi kuunguza.
Mwalimu yule alinijibu kitu ambacho mpaka leo sijawahi kukisahau.
Aliniambia wanaokoseaga wote ni wazoefu. Akatoa mfano kwamba fundi umeme ambaye siyo mzoefu anakuwa na umakini mkubwa, hivyo ni nadra akapigwa shoti. Lakini fundi umeme mzoefu anachukulia vitu kwa mazoea na hivyo kuwa rahisi zaidi kupigwa shoti.

Nimekuwa naliona hili kila mara, hasa kwenye huduma ya ukocha ninayoitoa. Kadiri mtu anavyoamini tayari anakijua kitu, ndivyo anavyokuwa mbovu kwenye kitu hicho.
Kadiri mtu anavyoona tayari ana uzoefu, ndivyo anafanya kwa mazoea na ubovu mkubwa zaidi.

Kwa kifupi ujuaji mwingi ni kikwazo kwa mafanikio makubwa.
Huwezi kufanikiwa kama unajiona tayari unajua kila kitu.
Na hata ikitokea umefanikiwa, mtazamo huo utakuletea anguko kubwa sana.

Mafanikio makubwa yanahitaji unyenyekevu, utayari wa kujifunza mara zote, hata kama unaona unakijua kitu.

Tukiangalia mfano wa kampuni kama ya Amazon, umekuwa ni msimamo wa Jeff Bezos kwamba kila siku inapaswa kuchukuliwa kama siku ya kwanza ya kufanya kitu ambacho kimekuwa kinafanywa kila siku.
Mtazamo huo unaondoa mazoea na ujuaji mwingi.
Mtu anakuwa tayari kujifunza na kujaribu vitu vipya kila mara.

Kama unataka kufanikiwa zaidi ya pale ulipo sasa, weka ujuaji pembeni na kuwa mnyenyekevu. Kila wakati fanya kama ndiyo mara ya kwanza na kuwa tayari kukifunza na kujaribu vitu vipya.

Hatua ya kuchukua leo;
Angalia ni maeneo gani ya maisha yako ambayo umekuwa unajiona tayari unajua kila kitu. Angalia pia ni maeneo gani umekuwa unajiambia tayari una uzoefu wa kutosha.
Na kuanzia sasa, chukulia kila siku kama siku yako ya kwanza kufanya kitu. Jifunze kwa kina na jaribu vitu vipya. Hayo yatakuwezesha kuondokana na ujuaji unaokuwa kikwazo kwa mafanikio yako makubwa.

Tafakari;
Huwezi kujifunza kitu ambacho tayari unadhani unakijua. Hivyo hatua ya kwanza muhimu kwenye kuishi maisha ya kujifunza endelevu ni kujua hujui ili kuwa tayari kujifunza.

Kocha.