2525; Mbadala Ndiyo Unaokuponza.

Kadiri unavyokuwa na machaguo mengi, ndivyo inavyokuwa vigumu kwako kuchukua hatua.

Pale unapokuwa na mbadala wa chochote unachofanya, ukikutana na ugumu utakimbilia kwenye mbadala huo.

Hiki ni kikwazo kikubwa kwa mafanikio ya wengi, kuwa na mbadala kunawafanya wasikomae na kitu kimoja mpaka wakapata matokeo makubwa.

Kujua wana mbadala au machaguo mengine hawajitoi kweli kweli kwenye kitu kimoja mpaka kikazaa matunda.

Ndiyo maana pamoja na wingi wa fursa ambazo zipo, bado watu hawafanikiwi.
Kwa sababu mafanikio hayatokani na fursa, bali namna unavyozifanyia kazi fursa hizo.

Hatua ya kuchukua;
Unapochagua kufanya kitu, achana na machaguo mengine na mbadala wowote ule. Jua ni kile tu ulichochagua ndiyo kipaumbele pekee kwako. Weka juhudi zako zote na umakini wako wote kwenye kitu hicho. Haijalishi unapitia magumu kiasi gani, usiangalie pembeni kutafuta mbadala, wewe komaa na kile ulichochagua.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa kwenye maisha.

Tafakari;
Kadiri unavyokuwa na machaguo mengi, ndivyo inavyokuwa vigumu kufanya maamuzi. Pale unapokuwa na mbadala, hutaweza kukomaa na kitu kimoja mpaka kikupe matokeo.

Kocha.