#SheriaYaLeo (34/366); Lengo Kuu Moja.
Unapochagua kufanya kazi chini ya mtu ambaye amebobea ili ujifunze kwake, lengo lako kuu ni kujifunza na siyo kulipwa vizuri au kupata hadhi kubwa.
Unachohitaji ni kujijengea ujuzi bora na wa kipekee, ambao utaweza kuutumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
Unapokuwa kijana na ndiyo unaanza kujenga taaluma au biashara yako, fanya kazi kujifunza na siyo kufanya kazi kulipwa.
Hiyo ina maana kama kuna fursa mbili mbele yako, moja inalipa vizuri lakini hujifunzi na nyingine inalipa kidogo ila unajifunza mengi, chagua fursa hiyo inayolipa kidogo lakini unajifunza.
Kila unachojifunza ni uwekezaji ambao utakulipa sana baadaye kama utaweza kuutumia vizuri.
Kujifunza ndiyo uwekezaji ambao huwezi kuupoteza kwa namna yoyote ile.
Watu wanaweza kukuibia au kukudhulumu mali zako, lakini hakuna anayeweza kukuibia ujuzi na uzoefu wako.
Kumbuka lengo lako kuu ni kujifunza na hivyo tumia kila fursa kuweza kukamilisha hilo.
Jijengee ujuzi na uzoefu ambao unaweza kuutumia kufanya makubwa zaidi baadaye.
Sheria ya leo; Ujuzi na uzoefu mkubwa ni bidhaa yenye thamani kubwa kwenye kazi na biashara. Pima kila fursa unayokutana nayo kwa kigezo kimoja, nafasi ya wewe kujifunza na kukua zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu