#SheriaYaLeo (56/366); Endelea kutanua mipaka yako.

Unapoianza safari ya kujifunza ili kuelekea kwenye ubobezi wa hali ya juu, unakutana na ukweli ambao hukuwa unaujua.
Ukweli huo ni safari hiyo ni ngumu na vikwazo ni vingi.
Kikwazo kikubwa kabisa kitakuwa ni kupata watu sahihi kujifunza kutoka kwao ili kuweza kufikia ubobezi.
Ili kuweza kuendelea na safari hiyo na kufikia ubobezi, lazima ujitoe sana kwenye kujifunza.

Unapoingia kwenye safari hii, unaanzia hatua ya chini kabisa. Hiyo ni hatua ngumu kwa sababu inakuwa vigumu kupata watu na maarifa sahihi, kwa kuwa hakuna anayekujua.
Kama hutakuwa umejitoa kweli kufikia ubobezi, utakubaliana na hali hiyo na kubaki kwenye ngazi hiyo, hasa kama unatokea kwenye hali ngumu.

Ili kufikia ubobezi, lazima uvuke kila hatua unayofikia kwa kuendelea kutanua wigo wako wa maarifa na ujuzi.
Utaweza kufanya hivyo kwa njia nne.

Njia ya kwanza ni vitabu, ambavyo ni rahisi kupata kwenye zama tulizopo sasa.
Wajibu wako ni kujua maarifa yapi unayoyahitaji ili kupiga hatua zaidi na kuhakikisha unayapata.

Njia ya pili ni kupata mawazo mapya yanayoendelea kugunduliwa kwenye eneo unalojijengea ubobezi.
Haya utayapata kupitia tafiti mbalimbali za eneo husika.
Hivyo ni muhimu sana ufuatilie machapisho na ugunduzi mwingine unaoendelea.

Njia ya tatu ni kupitia watu waliobobea kwenye eneo ulilochagua.
Hao pia wana viwango mbalimbali vya ubobezi, unapoanzia chini kabisa unaoweza kuwafiki ni wenye ubobezi wa chini.
Unahitaji kuweka juhudi ili uweze kuwafikia wenye ubobezi wa juu na ujifunze kutoka kwao pia.
Kila unapofikia hatua fulani, tafuta walio hatua ya juu zaidi na kujifunza kutoka kwao.

Njia ya nne ni mafunzo yoyote unayoweza kupata kwenye eneo ulilochagua.
Yanaweza kuwa mafunzo rasmi kama kozi mbalimbali au yasiyo rasmi kama kuhudhuria semina na mikutano mbalimbali.

Ili kufikia ubobezi wa juu, hupaswi kuridhika na hatu yoyote unayokuwa umefikia. Badala yake jisukume kukua zaidi kwa kutanua wigo wako na kujifunza vitu vipya kila wakati.

Sheria ya leo; Kila wakati kuwe kwenye kujifunza endelevu. Kila unapojiona umefika ngazi fulani na kuanza kuridhika nayo, jisukume kwenda ngazi ya juu zaidi, kwa kujifunza vitu vipya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu