2562; Kuna kitu hakipo sawa.
Kwa asili, mtoto akizaliwa anatakiwa aendelee kukua. Nguvu ya ukuaji tayari ipo ndani yake.
Kama mtoto hakui vizuri, kuna kitu kinazuia au kuathiri ile nguvu iliyo ndani yake.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kazi na biashara. Kadiri muda unavyokwenda, kile unachofanya kinapaswa kukua zaidi. Nguvu ya ukuaji tayari ipo ndani yako na pia ipo ndani ya kile unachofanya.
Kama kitu hakikui, kuna shida mahali.
Kama unaweka juhudi kukuza unachofanya lakini hakikui, maana yake kuna wengine ambao wanaweka juhudi kuzuia kisikue.
Au huwezi kujudi kabisa hivyo ile nguvu ya ukuaji iliyopo ndani haitumiki vizuri.
Changamoto nyingi zinazoathiri kitu kisikue zinatokana na juhudi kutokuwekwa kwa usahihi au juhudi pinzani kupata nguvu zaidi.
Kama biashara inapitia changamoto kubwa na haikui, kwa sehemu kubwa juhudi sahihi haziwekwi, yaani mmiliki haweki umakini mkubwa.
Au juhudi za makusudi za kuirudisha nyuma zinawekwa, kama watu kuiba au kuwafukuza wateja kwa huduma mbovu.
Mara zote jua asili ya kitu ni nini na pale ambapo matokeo yanaenda kinyume na asili, jua kuna tatizo mahali.
Usiridhike tu, badala yake tafuta tatizo lilipo, litatue ili uweze kusonga mbele.
Na tatizo gumu zaidi ni lile linalokuwa linaanzia ndani yako. Huwa tunakuwa na upofu wa madhaifu yetu wenyewe hivyo inahitajika juhudi kubwa sana kuweza kuvuka hilo.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jiulize asili yake ni nini na kinapaswa kuendaje. Kisha angalia kimekuwa kinakwendaje, kama ni tofauti na asili, jua kuna kikwazo mahali. Tatua kikwazo hicho ili uweze kupiga hatua kubwa.
Tafakari;
Nguvu ya asili huwa haifi, badala yake inalala au kutumika kwa namna nyingine. Kama hunufaiki na nguvu zako za asili, haimaanishi umezipoteza, zipo, ila tu hujaweza kuzitumia vizuri.
Kocha.