2581; Ujuaji mwingi.

Hakuna kikwazo kikubwa kwenye safari ya mafanikio kama ujuaji mwingi.

Ukishaanza kujiambia tu kwamba tayari unajua vitu fulani hivyo huna haja ya kujifunza tena au kuzingatia, jua umeanza kuanguka.

Ukishaona unajua kila kitu na huna kipya cha kujifunza, jua anguko lako halipo mbali.

Katika zama hizi za mabadiliko makubwa na yanayotokea kwa kasi, kujifunza endelevu ni hitaji la msingi kabisa ili uweze kufanikiwa.

Kiashiria kizuri kwamba unajifunza ni kuweza kuona jinsi ambavyo mawazo yako ya nyuma hayakuwa sahihi.
Unapokuwa unajishangaa kwa namna ulivyokuwa unafikiri na kuamini.
Hicho ni kiashiria kwamba unakua zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Haijalishi umefika hatua gani, kujifunza endelevu kunapaswa kuwa kitu kisichobadilika.
Kila wakati jisukume kujifunza vitu vipya kwenye kile unachofanya.
Pokea mawazo mbadala na hata usiyokubaliana nayo, yachunguze bila kuyahukumu.
Chagua ya kufanyia kazi kwenye kila unachojifunza.

Tafakari;
Siku unayoona tayari unajua kila kitu ndiyo siku unayokuwa umeanza anguko lako.
Kiu ya kujifunza haipaswi kukauka kwako kama unataka kupiga hatua kubwa.

Kocha.