Rafiki yangu mpendwa,

Kauli ya mwaka mpya mambo mapya ni kauli yenye msisimko mkubwa.
Kauli inayoamsha hamasa na shauku kubwa.

Ila kwa bahati mbaya sana hamasa na shauku hiyo huwa haidumu kwa muda mrefu.

Na hayo sijasema mimi, bali ni matokeo ya tafiri zilizofanywa karibu dunia nzima.

Tafiti hizo zilikuja na majibu ya kusikitisha sana.
Kwamba tarehe 19 mwezi wa kwanza kwenye kila mwaka ndiyo watu wanaachana na malengo yao ya mwaka mpya.

Na wala sihitaji kutumia nguvu nyingi kukuaminisha hizi tafiti.
Wewe jiangalie mwenyewe.
Je ile kasi uliyoanza nayo mwaka mpya ndiyo unayo mpaka sasa?

Kuwa tu mkweli kwako, jinsi ulivyojiambia mwaka huu utafanya makubwa, na kweli kuanza, umeishia wapi sasa?

Rafiki, siandiki hapa kukuhukumu, au kukufanya ujione hufai.
Huo ndiyo ubinadamu, kutaka kitu na kukipata ni vitu viwili tofauti kabisa.

Naandika hapa kukusaidia uvuke pale ulipokwama na kuanguka.

Baada ya jaribio lako la kwanza kuchemka, kwa kushindwa kuendelea na malengo makubwa uliyokuwa nayo kwa mwaka mpya, nina pendekezo dogo ambalo nataka nikupe.

Ukikamilisha pendekezo hili, mwaka wako utakwenda vizuri mno na hakuna kitakachokukwamisha usifanye makubwa.

Je upo tayari kwa pendekezo hilo?
Na je upo tayari kwa ajili ya pendekezo hilo?

Kama jibu ni ndiyo, basi endelea kusoma hapo chini.

Hatua ya kwanza.

Fikiria siku ya mafanikio kwako, siku ambayo umeimaliza na kuifurahia kweli, ukijiambia hii imekuwa siku bora na kamilifu kwako.

Chukua kalamu na karatasi kisha andika kila ulichofanya kwenye siku hiyo na muda ambao umekifanya.
Orodhesha kila kitu bila kuacha hata kimoja.

Andika muda ulioamka, umefanya nini baada ya kuamka na endelea na mfululizo huo mpaka muda unaenda kulala.

Hiyo ndiyo siku ya mfano kwako, siku ya mafanikio makubwa kwako.

Hatua ya pili.

Weka siku yako ya mfano kwenye uhalisia.
Kwa siku moja tu, iishi siku yako ya mfano kwa ukamilifu wake.

Fanya kila kitu kama ulivyoorodhesha na kupanga kufanya.
Usiache hata kimoja, fanya kile ulichopanga.

Hata kama unaona ni ngumu kiasi gani, wewe jiambie tu ni siku moja.
Usiangalie unafanya kwa miaka mingapi, bali angalia ni kwa siku moja tu.

Hatua ya tatu.

Rudia zoezi hilo kwenye kila siku mpya unayoipata, ukiiangalia siku hiyo tu kama ndiyo inayohitajika kufanya hivyo.

Usiangalie ni kwa siku ngapi utafanya, bali angalia leo unapofanya.

Ishi siku yako ya mafanikio siku moja kwa wakati.
Na baada ya muda, utashangaa jinsi maisha yako yanakuwa yamebadilika bila ya kuhangaika sana.

Kitabu cha rejea.

Najua unaweza kuwa na maswali mengi ya vitu gani ufanye kwenye siku yako hiyo, uamke saa ngapi, ulale saa ngapi n.k.

Majibu yote hayo yapo kwenye kitabu cha KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO.
Ni kitabu muhimu sana kwako kupata mwongozo wa kuiishi kila siku kwa mafanikio makubwa na kuweza kuwa na maisha ya mafanikio pia.

Jipatie nakala yako ya kitabu cha KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO kwa kuwasiliana na namba 0752 977 170 kupata maelekezo ya kukipata.

Usikubali mwaka wako upotee mapema hivi, sahau kuhusu mwaka na weka mkazo kwenye siku. Lazima utakuwa na siku bora kabisa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.