2585; Mteja yuko sahihi.
Unapokuwa kwenye biashara, hii ni kauli unayopaswa kuielewa kwa kina sana.
Kwamba mteja yupo sahihi mara zote.
Hata kama kwa upande wako unaona hayupo sahihi, jua kwa upande wake anajiona yupo sahihi.
Na kwa kuwa yeye ndiye anayefanya maamuzi iwapo anunue au la, na anunue kwako au kwa mwingine, ni muhimu uende naye katika huo usahihi wake.
Biashara yoyote ile ni kama burudani, lengo kuu likiwa kumfanya mteja ajisikie vizuri.
Kumfanya mteja ajione yuko sahihi ni moja ya njia za kumburufisha.
Una bidhaa au huduma bora kabisa ambayo unajua itamsaidia mteja wako.
Lakini mteja huyo kuna kitu anaamini au kusimamia ambacho unajua siyo sahihi.
Na kwa kusimamia hicho ndiyo anaweza kufanya manunuzi.
Kibinadamu utasukumwa kumwonyesha mteja kwamba hayupo sahihi, ukiamini unamsaidis.
Kinachotokea ni unampoteza mteja huyo.
Kwa kifupi, usiruhusu tofauti za imani, utamaduni na mengine yoyote yawe kikwazo kwa mteja wako kununua unachouza.
Kubaliana na chochote anachoona ni sahihi, kama tu yuko tayari kununua.
Kama bado hujaelewa ni kama mteja anaamini 1 + 1 = 4 ndiyo aweze kununua, basi yupo sahihi kabisa. Kubaliana naye na mshawishi kununua.
Usianze kuhangaika kumwonyesha kwa nini hayupo sahihi, wewe siyo mwalimu wa hesabu, wewe ni mfanyabiashara na kazi yako kuu ni kuuza.
Hatua ya kuchukua;
Fikiria ni mara ngapi umepoteza wateja kwa sababu tu ya kutaka kuwaonyesha hawapo sahihi. Je hiyo ilikusaidia nini? Maana walienda kununua kwingine na kuendelea kuamini kile walichoamini ni sahihi.
Kuanzia sasa weka mkazo kwenye mauzo, chochote anachoamini mteja ni sahihi kama yupo tayari kununua.
Tafakari;
Ukishakuwa kwenye biashara, imani, itikadi, siasa, ushabiki na mengine ambayo yanagusa hisia za watu, hupaswi kuyaendea kwa hisia. Badala yake kuwa tayari kukaa upande wa mteja mara zote.
Biashara ni kama maigizo, igiza uwezavyo ili uweze kufanya mauzo.
Kocha.