#SheriaYaLeo (102/366); Kupata Unachotaka, Wape watu kile wanachotaka.

Katika safari yako ya mafanikio, kuna mengi unayoyahitaji kutoka kwa watu wengine.
Hapo ndipo wengi huwa wanajisahau na kudhani watu wana wajibu wa kuwapa kile wanachotaka.

Lakini hivyo sivyo binadamu tulivyo.
Sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunajali zaidi mambo yetu kuliko mambo ya wengine.

Watu huwa hawakosi usingizi wakifikiria watawanufaishaje wengine, bali wanakosa usingizi wakifikiria watanufaikaje wao wenyewe.

Hivyo pale unapotaka watu wakupe kitu fulani, anza kwanza kuwapa wao kile wanachotaka.
Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuwaweka watu kwenye wajibu wa kukupa unachotaka.

Hata kama watu wanaonekana wana mamlaka na mafanikio kiasi gani, usidanganyike kwamba hakuna wanachotaka na wapo tayari kukupa wewe kile unachotaka.
Hata kama wanajinadi hivyo, usidanganyike, asili ya binadamu haibadiliki.
Wape watu kile wanachotaka na wao watakuwa tayari kukupa kile unachotaka.

Huu ndiyo msingi mkuu wa kwenye kazi, biashara, mahusiano na maisha kwa ujumla.
Kila mtu anaangalia zaidi maslahi yake binafsi.
Jali maslahi ya watu na wao watajali maslahi yao.
Wajibu wako mkubwa ni kujua maslahi ya wale unaoshirikiana nao, ili uyape kipaumbele na wao wayape maslahi yako kipaumbele.

Sheria ya leo; Pale unapokuwa unahitaji kitu chochote kutoka kwa wengine, anza kwa kuwapa kile wanachokihitaji kwanza. Wanufaishe kwanza watu kabla hujataka kunufaika nao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji