2606; Washindani siyo shida.

Watu wengi huona ushindani ni hatari kubwa kwenye biashara, au kitu kingine chochote.
Huona uwepo wa washindani utawaondoa kabisa kwenye kitu hicho.

Kufa kwa biashara au kitu chochote kile huwa hakusababishwi na udhindani, bali ni udhaifu wa ndani.
Japo kwa nje ushindani ndiyo utaonekana umesababisha, lakini ukweli ni udhaifu wa ndani ndiyo chanzo kikuu, ushindani umemalizia tu.

Kuwepo kwa ushindani ni kiashiria kizuri kwamba uhitaji wa kitu hicho upo.
Wajibu wako unakuwa ni kuwapatia watu kitu hicho ambacho tayari wanakihitaji, kwa namna ambayo hawawezi kupata kwa wengine.

Wateja hawalazimishwi kwenda kununua sehemu fulani, ila wanakwenda kwa mapenzi yao binafsi, kulingana na kile wanachokipata.

Hivyo kama mshindani anapata wateja wengi kuliko wewe, kama anawachukua wateja wako, jua hatumii mabavu kuwalazimisha waende kwake, bali kuna kitu anawapa na wewe huwapi.

Kama biashara yako itakufa kwa sababu washindani wanachukua wateja wako, siyo washindani wameiua, bali udhaifu wa biashara yenyewe, kushindwa kuwapa wateja kile wanachotaka ndiyo kimeiua.

Badala ya kuhofia ushindani unapaswa kuufurahia, kwa sababu unakutengenezea wateja ambao ni rahisi kuwachukua kama utawapa kile wanachotaka kwa namna ambayo hawajawahi kupata.

Hatua ya kuchukua;
Kwa biashara au chochote unachofanya, jiulize nani washindani wako? Nini ambacho wateja wanapata kwa washindani wako ila kwako hawakipati? Nini unawapa wateja wako ambacho hawawezi kupata kwa wengine?
Kama unajiambia huna washindani, basi hujui kile unachofanya na hiyo ni hatari zaidi.

Tafakari;
Mafanikio yapo kwenye kuwapa watu kile wanachotaka na kuna wengi watakuwa wanafanya hivyo, kitu ambacho ni kizuri kwa sababu kinakuza soko. Ukiwa na mbinu bora inakuwa rahisi kuteka soko hilo na kupata manufaa makubwa. Ukiwa dhaifu unapotezwa.

Kocha.