#SheriaYaLeo (112/366); Usiwaonee huruma maadui.
Maadui zako hawakutakii mema.
Kitu pekee wanachotaka kuona ni wewe ukishindwa na kuanguka kabisa.
Hivyo watafanya kila mbinu kuhakikisha wanakamilisha hilo.
Katika kukabiliana na maadui zako, kamwe usiwaonee huruma.
Pale unapoelekea kuwashinda wanaweza kutumia mbinu hiyo ya kutaka huruma kwako.
Kwa kuonyesha wamesalimu amri na kuomba muyamalize kwa mazungumzo.
Usikubali kunasa kwenye huo mtego.
Adui hafanyi hivyo kwa sababu anataka kweli myamalize.
Anafanya hivyo kwa sababu amezidiwa.
Hivyo anataka apate muda zaidi wa kwenda kujipanga ili alipe kisasi baadaye.
Adui yeyote unayemshinda anakuwekea kinyongo.
Anaendelea kutafuta fursa ya kuja kulipa kisasi na kukuangusha vibaya.
Ndiyo maana hupaswi kumwonea huruma adui, unapaswa kummaliza kabisa.
Adui ni sawa na cheche ya moto kwenye nyasi kavu.
Hata kama ni ndogo kiasi gani, inaweza kuleta madhara makubwa.
Ndiyo maana huwezi kuidharau cheche ya moto, bali unapaswa kuizima kabisa.
Kummaliza kabisa adui haimaanishi kumuua.
Bali inamaanisha kuondoa kila fursa anayoweza kutumia kulipa kisasi.
Kumwacha akiwa dhaifu kiasi kwamba hawi hatari tena kwako.
Lakini pia kuendelea kumweka kwenye udhibiti ambao hawezi kuwa na madhara kwako.
Kwenye maisha na safari ya mafanikio hupaswi kutengeneza maadui kwa makusudi.
Lakini kitendo tu cha wewe kuchagua kuyaishi maisha yako, kuna watu hawatafurahia hilo, hivyo watajenga uadui na wewe.
Ukishawajua hao, usiwaonee huruma wala kuwadharau.
Badala yake hakikisha unawadhibiti na kutokuwapa fursa yoyote ya kuleta madhara kwako.
Sheria ya leo; Wachukulie maadui kwa umakini mkubwa, ukiangalia historia yao ya nyuma. Wakati mwingine ni vyema kuwageuza kuwa marafiki ili kuwatuliza. Lakini kwa wengine hilo halifai, hivyo unapaswa kuwadhibiti na kuwaondoa bila ya huruma.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji