2782; Anaringa.
Kwenye maisha, watu wanataka uwe vile wanavyotaka wao, ukiwa tofauti, watakupa kila aina ya shutuma.
Lakini sasa, kwenye hii safari ya mafanikio, huwezi kuwa vile ambavyo kila mtu anataka uwe.
Badala yake unapaswa kuwa na misingi ambayo unaisimamia wakati wote, hata kama haiwafurahishi wengine.
Maana kama kuwafurahisha wengine ndiyo kungekuwa kunaleta mafanikio, basi kila mtu angekuwa amefanikiwa.
Lakini sivyo uhalisia ulivyo, kadiri unavyotaka kuwafurahisha wengine, ndivyo unavyojizuia kufanikiwa.
Mafanikio yatakutaka uwaudhi wengine, kwa namna ambapo watakuchukia kwa kile unachosimamia.
Uzuri ni kwamba watakuheshimu kwa kile unachosimamia.
Siku chache zilizopita nilipata nafasi ya kuzungumza kwenye kongamano la vijana. Jina la kongamano hilo liliitwa KONGAMANO LA VIJANA WAPAMBANAJI.
Huwa siyo mshiriki sana wa aina hii ya makongamano, ila mwandaaji aliponishirikisha nia yake na kuonyesha hali hiyo ya UPAMBANAJI, na kwa kuwa napenda sana mapambano ya mafanikio, niliona ni kitu kizuri kwangu na ninaweza kuwa na mchango kwa wengine.
Hivyo nilipopewa nafasi ya kuzungumza, nilielezea uhalisia wa kupambana kwenye eneo la biashara, kama njia ya uhakika ya kufika kwenye mafanikio makubwa.
Nilieleza wazi kwamba siyo njia rahisi, lakini mtu akiamua na kujitoa kweli, lazima atapata matokeo mazuri.
Na nikawapa kanuni moja kuu ya kufanyia kazi kwenye eneo la biashara ambayo itaenda kuleta mapinduzi makubwa kwao.
Nilipofika mwisho wa mazungumzo, washiriki waliomba nitaje namba yangu ya simu.
Niliwaeleza wazi sitafanya hivyo.
Nikawaambia kama kuna anayehitaji huduma yangu ya ukocha, basi apitie kwa mwandaaji wa kongamano hilo ili yeye amdhamini ndiyo niweze kufanya naye kazi.
Niliwaeleza kwa sasa sifanyi kazi na mtu ambaye hajaletwa kwangu na mtu ambaye tayari ninamwamini.
Nikawaambia kwenye huduma yangu ya ukocha siangalii sana mtu analipa nini, bali cha kwanza kuangalia ni kama mtu yupo tayari kufanya, kwa kujituma zaidi ya alivyozoea.
Mimi kwangu niliona ni kitu cha kawaida kabisa, maana ndiyo msimamo wangu kwenye huduma ninazotoa.
Lakini ilileta taharuki kubwa, maana wazungumzaji wengine wote walikuwa wanatoa namba zao baada ya kuzungumza.
Hivyo wakaanza kusema wazi kwamba ninaringa, kwa nini nisitoe namba, kwa nini niache wateja ambao wanataka huduma.
Hilo halikunitikisa hata kidogo, bali lilinifanya nione limekuwa na msaada zaidi.
Unafikiri mtu ambaye anaweza kukubali kukosa namba yangu kirahisi hivyo anaweza kuhimili safari ya mafanikio?
Mtu ambaye kikwazo kimoja rahisi kama cha namba kinamzuia atauweza moto wa mafanikio?
Sasa kitu kizuri zaidi, katika kongamano hilo hilo, alikuja mshiriki mmoja na kuniambia najua umeshatoa utaratibu wa jinsi ya kupata huduma yako, kwa kupitia kwanza kwa mwandaaji wa kongamano, ila mimi naihitaji kweli na nipo tayari kufanya chochote kuipata.
Nikamwambia aanze kwa kusoma vitabu vyangu viwili, akachukua hatua hiyo na sasa tupo kwenye mchakato wa yeye kuingia kwenye huduma.
Utakapojiwekea misingi ambayo unaisimamia, watu watakushutumu kwa kila namna.
Kama huna ngozi ngumu ya kuvumilia na kupuuza shutuma hizo, hutaweza kupata mafanikio unayoyataka.
Hatua ya kuchukua;
Ni shutuma gani ambazo watu wamekuwa wanakupa pale unaposimamia misingi yako uliyojiwekea kwenye safari yako ya mafanikio?
Umekuwa unavuka au kupuuzaje shutuma hizo ili zisiwe kikwazo kwako?
Ni lazima uwe na ngozi ngumu sana ili kufanikiwa.
Tafakari;
Mafanikio yangekuwa rahisi, kila mtu angekuwa nayo.
Siyo rahisi na ndiyo maana wengi hawajayapata.
Hivyo kila unapotaka kukimbilia kufanya vitu rahisi, jikumbushe hili na ufanye maamuzi sahihi.
Kutaka kuwafurahisha watu ni maamuzi sahihi.
Kusimamia misingi sahihi ni maamuzi magumu.
Unajua kipi kinaweza kukupa mafanikio hapo.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed