2814; Acha kujikwamisha.

Ni jambo la kushangaza, lakini ndivyo uhalisia ulivyo, umekuwa unajikwamisha sana wewe mwenyewe.

Pale mambo yanapokwenda vizuri kabisa kwa upande wako, unayaingilia na kuyavuruga.
Unaharibu kile ambacho tayari kilishakuwa cha uhakika kwa kushindwa tu kuwa na utulivu na msimamo.

Kutaka kwako vitu vipya na vinavyosisimua kunakufanya uharibu vitu vya uhakika ambavyo ulikuwa umeshavijenga.

Umejenga biashara yako kutoka chini, umepambana nayo mpaka imeanza kusimama.
Cha kushangaza unakuja kutoa fedha kwenye biashara hiyo na kwenda kujaribu mambo mengine yasiyokuwa na uhakika.
Umeingiwa tamaa na vitu unavyohadaiwa vinalipa sana, mwishowe unapoteza kila kitu.

Umeweka juhudi sana kwenye kitu mpaka kimesimama na hapo unaona huhitaji tena kuweka juhudi. Matokeo yake unaanza kupata anguko kubwa.

Hatua ya kuchukua;
Endelea kuheshimu kila ambacho kimekuwa na manufaa kwenye maisha yako. Kamwe usivuruge kitu ambacho tayari kina manufaa kwako. Utulivu na msimamo ni tabia muhimu sana kwa kujenga na kudumu kwenye mafanikio.

Tafakari;
Kuwa na mtazamo mbovu wa kifikra huchangia sana kuyavuruga mafanikio yako mwenyewe. Kwa kuwa mtazamo huo hautegemei mambo kuwa mazuri, unakusukuma ufanye mambo ya kijinga ili tu kuvuruga mazuri ambayo umeshayajenga.
Jijengee mtazamo bora wa kifikra ambao hauvurugi mafanikio yako.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed