2815; Jeshi la mtu mmoja.
Kikwazo kikubwa kabisa kwenye maisha yetu huwa kinaanzia kwenye fikra na mitazamo yetu.
Vile ulivyo sasa, ni matokeo ya fikra ambazo zimetawala akili yako kwa muda mrefu.
Moja ya mitazamo inayowakwamisha wengi kwenye safari ya mafanikio ni jeshi la mtu mmoja.
Mtazamo wa jeshi la mtu mmoja ni ile hali ya kuona unaweza kufanya kila kitu wewe peke yako.
Kwa vitu vidogo, ni kweli unaweza kufanya peke yako.
Lakini inapokuja kwenye vitu vikubwa, ambavyo vitakupa mafanikio makubwa, peke yako huwezi.
Unahitaji timu ili kuweza kukamilisha mambo makubwa.
Na kadiri unavyoyataka makubwa, ndivyo unavyohitaji timu kubwa zaidi.
Hakuna mtu amewahi kukamilisha chochote kikubwa duniani peke yake.
Wote waliofanya makubwa walikuwa na timu ambazo zilikuwa zimejitoa kweli kweli kukamilisha kile ambacho zilipaswa kufanya.
Usidhani itakuwa tofauti kwako.
Uhitaji wa timu hauwezi kukwepeka.
Kama unataka kufanya makubwa, jua wazi kabisa kwamba hutaweza kufanya peke yako.
Hivyo unapokuwa na ndoto na maono makubwa ya baadaye, anza kujenga timu yako mapema.
Maana timu haihitaji tu watu wa kuokoteza.
Bali inahitaji watu walioyaelewa maono, kuyakubali na kuwa tayari kuyapigania.
Kila kitu kwenye maisha ni vita, hakuna vita unaweza kushinda peke yako.
Na hata ukiwa na jeshi, hakuna aliye tayari kuteseka kama kitu hakina maana kwake.
Hapo unaelewa kwa nini unahitaji watu sahihi, wanaoyaelewa maono na kuwa tayari kuyapigania.
Uzuri ni kwamba, jeshi tayari lipo, linachosubiri ni kumpata jenerali sahihi wa kuliongoza kwenye mapambano sahihi.
Unapokuwa jenerali sahihi kwenye kile unachotaka, unawavutia wanajeshi sahihi kuja kwako na unapowaamini na kuwapa majukumu, wanakuwa tayari kupambana kufa na kupona ili kuleta ushindi.
Hatua ya kuchukua;
Futa kabisa fikra na mtazamo wa jeshi la mtu mmoja. Jua hakuna chochote kikubwa unachoweza kufanya peke yako. Kubali unahitaji timu, unahitaji jeshi linaloyaelewa maono uliyonayo na kuwa tayari kuyapambania.
Anza mapema kujenga timu yako hatua kwa hatua, itakusaidia kufikia ndoto kubwa ulizonazo.
Tafakari;
Kila kitu kwenye maisha ni vita.
Nenda kwenye vita yoyote peke yako na adui atakunywa damu yako kama supu.
Unahitaji timu, jeshi lililo tayari kupambana kweli kweli.
Jenga timu na jeshi lako, unalihitaji sana katika kufikia ndoto zako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed