2920; Lini mwisho wa kuuza?
Kwako rafiki yangu mpendwa unayesubiri kwa hamu siku ambayo biashara yako itakuwa kubwa na uwe umeajiri watu ili uache kuuza.
Watu wengi huwa hawayapendi mauzo, kwa sababu yanahusisha kazi kubwa na ya muda mrefu.
Hivyo huwa wanaisubiri kwa hamu siku ya mwisho kuuza.
Leo nina habari ambazo hazitakufurahisha sana.
Hakuna siku ya mwisho kwako kuuza.
Kama mmiliki wa biashara, mauzo ni kitu ambacho utakifanya maisha yako yote.
Kitakachobadilika ni unauza nini.
Wakati unaanza biashara, utafanya kazi kubwa ya kuuza bidhaa na huduma zako kwa wateja wako.
Kadiri biashara inavyokua ndivyo unaajiri watu wengi zaidi wa mauzo na kukusaidia jukumu hilo la mauzo.
Lakini hiyo haimaanishi kwamba ndiyo umefika mwisho wa mauzo.
Unahitaji kuendelea kujiuzia wewe mwenyewe ndoto kubwa ulizonazo ili uendelee kuzipigania bila ya ukomo.
Unahitaji kuwauzia wafanyakazi na washirika wako umuhimu wa kufanya yale unayowataka wayafanye kwa wakati unaotaka wafanye.
Unahitaji kuwauzia wauzaji wako umuhimu wa kuuza kile unachouza na kukikubali kama ndiyo kilicho bora kabisa na chenye manufaa kwa wateja walengwa.
Unahitaji kuwauzia wanaokusambazia bidhaa na huduma mbalimbali umuhimu wa kukupa kile unachotaka kwa wakati ili biashara yako iweze kwenda.
Unahitaji kuwauzia wahasibu na wanasheria mikakati uliyonayo ili wakupe ushirikiano mzuri kwenye maeneo yao.
Unahitaji kuwauzia mabenki, wakopeshaji na wawekezaji umuhimu wa kukupa mtaji wa kukuza biashara yako.
Kwa kuwa mauzo ni kitu ambacho hakina mwisho kwenye maisha yako ya kibiashara, ni vyema ukabadili mtazamo wako juu yake.
Kwanza kabisa unapaswa kuyapenda sana mauzo, kwa sababu ni kitu utakifanya maisha yako yote. Sasa utakuwa na maisha ya ajabu sana kama utakuwa unafanya kitu usichokipenda.
Mbili unapaswa kuwa bora kabisa kwenye uuzaji, ili uweze kuwa muuzaji bora kwenye kila eneo utakalokuwa unauza kwa maisha yako yote. Huwezi kujisikia vizuri wala kufanikiwa kama hujabobea kwenye kile unachofanya kila siku.
Kadiri unavyokuwa na ushawishi mkubwa ndivyo unavyokamilisha mauzo yako mengi.
Kila unachofanya kwenye biashara yako, jiulize kinachangiaje mauzo zaidi. Kwa sababu hilo ndiyo jukumu lako kuu kwenye biashara.
Watu wenye taaluma mbalimbali huwa wanatanguliza vyeo vya taaluma zao kabla ya majina yao.
Mfano Dr. Mwl. Eng. Arch. CPA. na kadhalika.
Leo nakupa ruhusa ya kutanguliza neno muuzaji kabla ya jina lako.
Kwa mfano kama jina lako ni Alex, basi unajiita Muuzaji Alex.
Kufanya hivyo kuna nguvu ya kukukumbusha kila wakati wajibu ambao utaufanya kwa maisha yako yote, hivyo unapaswa kuubobea kweli kweli.
Na kama muuzaji, kuna mauzo muhimu ya aina mbili unayopaswa kuyafanya.
Kwanza ni kujiuzia umuhimu wa wewe kufanya mauzo. Lazima ukubali kutoka ndani ya nafsi yako kwamba kweli unapaswa kufanya mauzo kwa maisha yako yote. Upokee, kukubali na kuyafanya mauzo kwa shauku kubwa.
Mbili ni kujiuza wewe mwenyewe kwako mwenyewe. Lazima ujikubali sana wewe mwenyewe na uone kweli uwezo wa kufanikiwa kwenye mauzo na biashara uko ndani yako.
Bila ya kujikubali wewe mwenyewe, hakuna kingine kikubwa utakachoweza kufanya kwenye maisha yako.
Walimu hufundisha,
Waandishi huandika,
Na wauzaji huuza.
Nenda kauze leo na kila siku.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe