2928; Asiwepo wa kuizidi biashara.

Rafiki yangu mpendwa,
Matatizo mengi ya kibiashara yamekuwa yanaanzia pale mfanyabiashara anaposhindwa kujitofautisha yeye na biashara yake.

Waanzilishi wengi wa biashara huwa wanadhani wao na biashara zao ni kitu kimoja. Na hilo limekuwa linapelekea wafanye maamuzi ambayo yanaiathiri sana biashara.

Kosa kubwa wanalofanya ni kuifanya biashara kuwa tegemezi kwao na kwa baadhi ya watu wengine.
Wanaifanya biashara ishindwe kujiendesha kama wao au watu fulani hawapo.
Watu hao wanaweza kuwa baadhi ya wafanyakazi, wateja au wasambazaji.

Sikiliza rafiki, wewe na biashara yako siyo kitu kimoja.
Biashara ni kitu kinachopaswa kujitegemea chenyewe.
Kitu kinachopaswa kusimama imara na kutotegemea uwepo wa watu fulani ndiyo iende.

Kwa maneno mengine hapaswi kuwepo mtu yeyote ambaye anaizidi au yuko juu ya biashara.
Mtu anayejiona kwamba bila uwepo wake basi biashara hiyo haipaswi kuwepo.
Hata wewe mwanzilishi wa biashara, unapaswa kuijenga biashara yako kiasi kwamba inaweza kujiendesha hata kama haupo kabisa.
Unapaswa kufika hatua ya kuweza kujifukuza kwenye biashara na ikaenda bila shida.
Ni hatua hiyo ndiyo unakuwa umefikia uhuru wa kweli kwenye biashara.

Usiruhusu mtu yeyote kuwa juu ya biashara yako, kwamba biashara haiwezi kwenda bila uwepo wake.
Na hilo linawezekana kwa kujenga mfumo wa kuendesha biashara.
Hakikisha mtu yeyote anaweza kuondolewa na bado biashara ikaenda vizuri tu.

Anza kwa kuondoa utegemezi wa biashara yako kwa mtu yeyote mmoja. Iwe ni mfanyakazi, mteja, mbia, msambazaji na wengine wote wanaojihusisha na biashara.
Kamwe usikubali kuwe na mtu yeyote mmoja ambaye ndiyo anakuwa anategemewa sana na biashara.
Yaani asiwepo mtu ambaye bila uwepo wake biashara haiwezi kwenda.

Watu huwa wana tabia ya kujenga kiburi pale wanapojua wanategemewa zaidi. Pale wanapoona biashara haiwezi kwenda bila wao, wanajiamulia namna ya kufanya mambo kwenye biashara.
Hapa ndipo unapopata wafanyakazi wanaojiamulia mambo wenyewe bila kufuata utaratibu, wateja wanaojipangia vile wanataka na hata wasambazaji wasiojali.

Wajibu wako namba moja ni kuhakikisha kila anayehusika na biashara yako anajua wazi kabisa anaweza kuondoka muda wowote na bado biashara ikaenda vizuri tu.

Na hilo litaanza kwa kuwafukuza wale wote wenye viburi. Kuanzia wafanyakazi, wabia, wateja na hata wasambazaji.
Wale wote wanaojiona bila wao biashara haiwezi kwenda, waondoe mara moja.
Halafu pambana biashara iweze kwenda bila wao.
Ukifanikisha hilo, wengine wanaobaki watakuwa na heshima kwa biashara na kufuata taratibu zote zilizopo.

Huenda una hofu kwamba ukiwaondoa baadhi ya watu basi biashara itakufa.
Hilo unapaswa kulifanyia kazi haraka kwa kuwaondoa kisha kujenga biashara isiyo na utegemezi.
Kwa sababu usipofanya hivyo sasa ili biashara isife, itakuja kufa tu huko baadaye, na watakaoiua ni hao hao unaowavumilia sasa.
Hivyo kutokuchukua hatua sasa siyo kwamba umetatua tatizo, bali umelisogeza mbele na unalifanya likue zaidi.

Kuendesha biashara ambayo kuna watu wanajiona bila wao biashara hiyo haiwezi kwenda ni kama umeshikwa mateka na watu hao. Utalazimika kufuata matakwa yao hata kama siyo sahihi.
Sasa hilo halikuwa lengo la wewe kuingia kwenye biashara.
Hukuingia kwenye biashara ili upangiwe nini ufanye na nini usifanye.
Uliingia kwenye biashara ili uwe huru kufanya maamuzi yoyote yale.
Linda sana uhuru huo kwa kuhakikisha wote wanajua wanaweza kuondoka kwenye biashara na bado ikaendelea.

Unapojenga biashara ni sawa na kujenga himaya au ufalme. Himaya huwa inakuwa na mfalme mmoja tu, ambaye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Hakuna mtu yeyote ambaye himaya haiwezi kwenda bila uwepo wake.
Hilo ni eneo muhimu sana la kuzingatia, ambalo litakufanya uwe huru.

Anza kwa kuwa na mbadala wa kila aliye kwenye biashara yako.
Asiwepo yeyote ambaye ndiyo kila kitu.
Kwa wafanyakazi kuwa na mbadala, kila jukumu kwenye biashara liweze kufanywa na mtu zaidi ya mmoja.
Kwa wateja, kuwa nao wengi kiasi kwamba akiondoka mmoja au wachache biashara haiathiriki sana.
Kadhalika kwa wabia na wasambazaji, ondoa utegemezi kwa mtu mmoja.

Kama unaona ukichukua maamuzi fulani sasa biashara itaathirika sana, ndiyo wakati sahihi wa kuyachukua kisha kupambana kuziondoa athari hizo kwenye biashara.
Kadiri unavyochelewa kuchukua maamuzi hayo ndivyo unavyofanya tatizo kuwa kubwa zaidi.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe