2933; Hatari ya saratani.

Rafiki yangu mpendwa,
Saratani huwa ni ukuaji wa eneo fulani la mwili usio na udhibiti wala ukomo.

Hatari kubwa ya saratani ni pale inapoachwa ikaendelea kukua.

Kadiri saratani inavyochelewa kuondolewa, ndivyo inavyokuwa na hatari kubwa.

Na ubaya wake ni inavyokua haibaki tu pale inapokuwa imeanzia, badala yake inasambaa kwenye maeneo mengine ya mwili.

Hivyo hata unapokuja kuitoa kwa kuchelewa, inakuwa haina maana kwa sababu inakuwa imeshasambaa sana.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha yetu.
Kuna saratani ambazo huwa zinajitokeza na hatari yake inakuwa kubwa kadiri tunavyochelewa kufanya maamuzi.

Inaweza kuwa ni tabia binafsi, unaanza na tabia fulani ndogo ambayo siyo sahihi, lakini huichukulii hatua.
Kinachokuja kutokea ni tabia hiyo inakuwa imekomaa na kuzaa tabia nyingine ambazo ni mbaya pia.

Au inaweza kuwa ni watu unashirikiana nao kama wafanyakazi. Mmoja anaanza kwenda kinyume na taratibu ulizoweka, wewe unamvumilia. Kinachokuja kutokea ni tatizo linakuwa kubwa na wafanyakazi wengine wengi wanakuwa wameungana naye.

Jambo lolote kwenye maisha yako linaloanza kidogo, unapolipuuza linakua na kuleta madhara makubwa zaidi baadaye.

Hivyo unapaswa kuwa kama daktari wa upasuaji, unapoiona saratani inaanza, usiisubirishe, ikate haraka sana kabla haijashika mizizi na kusambaa.

Kila tatizo lolote kubwa ulilonalo sasa halikuanza na ukubwa ambao upo sasa. Lilianza kidogo kidogo, wewe ukalipuuza na likaendelea kukua na sasa unaliona ni hatari.

Chukua mfano wa madeni, hakuna anayeanza akiwa na madeni makubwa ghafla. Bali tabia mbaya ndogo ndogo za kifedha zinajenga madeni madogo madogo mpaka mtu anajikuta kwenye deni kubwa.

Kadhalika kuwa na watu ambao hawakusikilizi na kukuheshimu.
Haikuanza mara moja, bali ilianza kidogo kidogo na wewe ukapuuza ukiona ni kitu kidogo.
Hatimaye kimeshika mizizi na kusambaa. Maana watu huambiana na kuigana kwenye yote wanayofanya.

Weka mipango na taratibu za mambo yote unayofanya.
Kisha pale kitu chochote cha tofauti kinapojitokeza, chukua hatua mara moja na kumalizana nacho.
Usiwe mtu wa kushindwa kufanya maamuzi.
Kumbuka kadiri unavyochelewa kufanya maamuzi, ndivyo tatizo linazidi kukua na kusambaa.

Hiyo haimaanishi ukurupuke na kutatua kila tatizo mara tu unapoliona. Lazima ujihakikishie kwa haraka tatizo ni nini na chanzo chake ni nini. Maana unaweza kukimbilia kuondoa kansa isiyo sahihi. Ukaacha tatizo likiendelea kushika mizizi licha ya kudhani umeshaliondoa.

Uongozi ni kuweza kufanya maamuzi haraka na kuyasimamia mpaka yalete matokeo bora.
Simama humo kama kiongozi wa biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Usijiendee tu kwa kufuata mkumbo.
Jua kila unachojihusisha nacho na namna kinapaswa kuwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe