2950; Yule kuku aliyekuwa anataga sana.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu kwenye maisha huwa kinakuja na tarehe ya mwisho wa matumizi.
Kwa Kiingereza wanaita expire date.
Kila kitu, ikiwepo mimi na wewe.
Na hiyo haimaanishi tu kifo, bali mwisho wa matumizi ya uzalishaji mkubwa.

Kama umewahi kufuga, unakumbuka kuku uliyekuwa naye, ambaye alikuwa anataga sana. Kila mtu alimpenda sana kuku huyo. Lakini nini kilitokea?
Alifika mahali akawa hatagi tena na hatimaye kisu kikampitia, akawa kitoweo.
Wakati anataga vizuri hukufikiria kumchinja, lakini alipoanza kutokutaga vizuri, hukufikiria mara mbili kumchinja.

Inawezekana pia ni ng’ombe umewahi kuwa naye, ambaye alikuwa anatoa maziwa mengi mno.
Alitunzwa vizuri kipindi hicho akitoa maziwa mengi. Lakini alipoanza kupunguza maziwa anayotoa, shoka lilimpitia bila huruma.
Hukujiambia ng’ombe huyu alikuwa anatoa maziwa mengi huko nyuma, wacha tumsubirie atatoa tena.
Ulijua vyema, wakati wake wa uzalishaji nzuri umepita, kilichobaki ni awe kitoweo.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mimea, huenda umewahi kuwa na miti ya matunda ambayo ilikuwa inazalisha matunda kwa wingi. Labda ni machungwa, maembe au mapapai. Mimea hiyo ilipoacha kuzalisha matunda kwa wingi, ilikatwa pale ilipoonekana ina matumizi bora zaidi kwa kukatwa kwake.

Somo kubwa sana tunalojifunza kwenye mifano hii ya asili ni kila kitu kina matumizi wakati kina uzalishaji mzuri.
Lakini kipindi cha uzalishaji kinapopita, kitu hicho huwanyiwa matumizi mbadala.
Hakuna anayesubiri kitu hicho kirudi kwenye uzalishaji wake, maana inafahamika haiwezekani kurudi tena.

Tunaelewa hilo kwenye asili, lakini tunashindwa kulielewa kwa watu.
Kuna watu huwa wanakuwa na uzalishaji mzuri sana kwa kipindi fulani.
Tunafurahishwa na uzalishaji wao, kwa kuwa unatunufaisha sana.
Tunakuwa tayari hata kuwapa upendeleo, kwa sababu ya matokeo mazuri wanayotupa.
Halafu wanafika hatua ambayo hawana tena uzalishaji kama wa awali.

Wakishafika hatua hiyo, hatukubali kwamba muda wao wa uzalishajiu umeisha. Bali tunasubiri warudi kwenye uzalishaji wao wa nyuma, kitu ambacho hakitokei.
Tunasubiri huku wakiendelea kuwa mzigo kwetu.
Tunachosahau au kushindwa kuelewa na kukubali ni kipindi chao cha uzalishaji kimepita na hakiwezi kurudi tena.
Hivyo kinachofuata ni kuondolewa kwenye nafasi zao ili wawekwe watu wengine wanaoweza kuwa na uzalishaji mkubwa.
Tunachelewa sana kufanya hivyo, mpaka tunapata hasara kubwa.

Hii inatokea kwa wafanyakazi wazuri unaoweza kuwa nao kwenye biashara yako. Kuna kipindi wanakuwa wazuri sana, wanazalisha kwa wingi na unafurahia.
Lakini baada ya muda uzalishaji wao unapungua sana. Badala ya kukubaliana na asili kwamba muda wao umekwisha, wewe unaendelea kung’ang’ana nao, ukitegemea watarudi kwenye ubora wao wa awali.
Kitu ambacho huwa hakitokei na inatugharimu.

Inaweza kuwa ni wateja, ambao awali walikuwa wazuri sana, wananunua kwa wingi na kulipa kwa wakati. Wakawa chanzo cha faida nzuri kwetu, tukawapenda na kuwategemea.
Halafu wanafika hatua hawawezi tena kununua kwa wingi na wanasua sua kwenye malipo. Unatumia uzoefu wao wa nyuma kuendelea nao na wanakuwa chanzo cha matatizo makubwa.

Hata kwa upande wa wasambazaji, unaweza kuwa na wasambazaji wanaofanya vizuri, wanakupa mali kwa wakati katika hali bora. Halafu wanaanza kukusumbua.

Na pia inaweza kuwa ni wewe mwenyewe. Mwanzoni ulikuwa na shauku na msukumo mkubwa vilivyofanya uweke juhudi kubwa kwenye biashara zako. Baadaye inakuwa ni kama taa imezimwa, shauku na msukumo vinazima ghafla.
Unaendelea kujisukuma na kujiburuza kwenye biashara hiyo lakini hakuna jema linalotokea.
Unakuwa umefikia kipindi cha mwisho cha matumizi kwenye aina hiyo ya biashara na unapaswa kujiondoa kabla hujaiangusha kabisa.
Unadhani kwa nini makampuni makubwa huwa yanawaondoa viongozi wake wa juu.
Au timu za mpira zinafukuza makocha wake.
Kwa sababu kipindi cha matumizi kwao, katika hali wanayokuwepo, kinakuwa kimeisha.

Inapokuja kwa watu na hata kwako mwenyewe, endeleza kipimo unachotumia kwa mimea na wanyama. Kuna kipindi kizuri cha uzalishaji ambapo unanufaika. Na kipindi hicho kinapopita, inapaswa kuondolewa. Kisu, panga au shoka vinahusu.
Ndiyo, kuna wakati tatizo la uzalishaji linaweza kuwa la muda mfupi tu, ila baadaye uzalishaji ukarudi.
Lakini wote tunajua pale ambapo uzalishaji umefika mwisho na hauwezi kurudi tena.

Inapokuja kwenye biashara yako na mengine yanayokuhusu, chukua hatua sahihi kwa watu na hata kwako pia.
Pale uzalishaji unapokuwa vizuri kuwa hata na upendeleo.
Lakini uzalishaji unapokuwa na ukomo, usiendelee kung’ang’ana na kitu.
Chukua hatua sahihi kwa wakati badala ya kuendelea kukumbatia hasara.

Kumbuka kila kitu huwa kinakuja na tarehe ya mwisho ya matumizi yake.
Kwa watu tarehe hizo hazijaandikwa usoni.
Bali utaweza kuzipima kwa mwenendo wa uzalishaji.
Fuatilia sana mwenendo huo kwa kila unayejihusisha naye na usisite kuchukua hatua sahihi.
Matokeo ya nyuma yasikuzuie kufanya maamuzi sahihi sasa.
Jaribu kufanya kila njia kumsaidia mtu kuboresha uzalishaji wake.
Pale inaposhindikana, basi jua muda wa mwisho wa matumizi umefika.
Na kinachofuata ni kisu, panga au shoka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe