Rafiki yangu mpendwa,

Fedha ndiyo kitu cha umuhimu kwenye maisha yetu baada ya pumzi, na hapo ni ukiwa mzima, kwani ukipata changamoto ya upumuaji, fedha inakuwa kitu cha kwanza kwako, kuhakikisha unapata matibabu ya kukuvusha kwenye hilo.

Fedha ndiyo kitu ambacho kila mmoja wetu anafikiria anapoamka, siku nzima na hata kabla ya kulala. Fedha inagusa kila eneo la maisha yetu.

Lakini cha kushangaza sana, kitu hiki muhimu zaidi, hatujawahi kukaa darasani na kufundishwa kwa umakini jinsi ya kwenda nacho kwenye maisha.

Hebu fikiria miaka 7 uliyokaa kwenye elimu ya msingi, miaka mingine 4 sekondari na huenda zaidi ya hapo kama ulifika elimu ya juu zaidi, umefundishwa mambo mengi. Umefundishwa historia za vita mbalimbali, umefundishwa wadudu na mimea, miamba na anga na hata miji mikuu ya mataifa mbalimbali.

Lakini kwa miaka yote hiyo zaidi ya kumi umekaa kwenye mfumo wa elimu, hebu niambie ni mara ngapi ulifundishwa kuhusu maana ya fedha, kuweka akiba, kuwekeza, kuwa na bajeti binafsi na kuhusu madeni?

Ni mara ngapi ulifundishwa kuhusu uwekezaji kwenye soko la hisa, vipande na hata hatifungani? Huwa sichezi kamari, lakini ninaweza kuweka dau kubwa kwamba tukiwachukua wahitimu 10 wa chuo kikuu na kuwauliza waelezee kuhusu uwekezaji wa hisa, vipande na hatifungani, 7 watashindwa kabisa. Na hiyo ni namba nzuri ninayoitoa, uhalisia unaweza kuwa mbaya zaidi ya hapo, huenda 9 wakashindwa kabisa.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, kitu muhimu ambacho tutahangaika nacho kwa maisha yetu yote hapa duniani, hatujawahi kufundishwa. Badala yake tumekuwa tunawaiga wale wanaotuzunguka, ambao nao hawajawahi kufundishwa, hivyo tunaiga makosa.

Ndiyo maana changamoto za kifedha kwenye jamii zinafanana kwa wote, bila ya kujali kipato. Yaani kwenye eneo moja, anayepata kipato cha laki moja kwa mwezi na anayepata cha milioni moja kwa mwezi, wote wana madeni, wote hawana akiba na wala hawana uwekezaji wa uhakika.

Nimekuwa nakataa kwamba changamoto za watu za kifedha hazianzii kwenye kipato wanachoingiza, bali zinaanzia kwenye mtazamo na maarifa waliyonayo kifedha.

Na hilo ndiyo nimepata nafasi ya kukuelezea kwa kina kwenye kipindi nilichofanya kwenye SIMULIZI NA SAUTI na Irene Kamugisha.

Kwenye kipindi hiki nimekushirikisha mambo yote ya msingi unayopaswa kuyajua kuhusu fedha ambayo ukiyazingatia utaweza kuondoka kwenye umasikini kwa kuongeza kipato, kuondoka kwenye madeni, kuweka akiba na kufanya uwekezaji.

Mwisho nimekushirikisha mambo 10 ya uhakika ambayo ukiyafanya, hatua kwa hatua, mwaka huu unaenda kuwa bora kabisa kwako kifedha.

Kipindi hicho kizuri kipo hapa chini, chukua kalamu na karatasi na kiangalie huku ukiandika yale ya muhimu unayokwenda kufanyia kazi.

Rafiki yangu mpendwa, naamini kipindi hiki kimekufungua kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la fedha. Nikusihi uanze kufanyia kazi mara moja yale uliyojifunza, ambayo ni mengi sana kwako kuweza kupiga hatua kifedha. Na kama utataka kuzama ndani zaidi, ili ufanye haya kwa uhakika zaidi, jipatie nakala yako ya kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Kupata kitabu wasiliana na 0752 977 170.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.

www.amkamtazania.com | www.mauzo.tz